Polisi yaonya vitisho, uzushi Uchaguzi Mkuu
JESHI la Polisi limeagiza wananchi wajiepushe na lugha za vitisho, matusi na uchonganishi wakati huu wa mchakato wa Uchaguzi Mkuu.
Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime amesema hayo alipozungumza katika kipindi cha Power Breakfast
kilichorushwa na Kituo cha Redio cha Clouds FM.
“Kila mtu afuate sheria, Polisi tutafuata sheria, wananchi, mwanasiasa wafuate sheria. Tuache lugha za
vitisho, matusi, uchonganishi na kusambaza taarifa za uongo kwenye mitandao,” alisema Misime.
Aliongeza: “Taarifa za uzushi, kutukana na kutengenezea watu sauti zionekane zimetoka kwa mtu fulani, tukiepuka hayo yote uchaguzi wetu kama ilivyo kawaida utakuwa wa amani”.
Misime pia alitoa mwito kwa wanasiasa kuzingatia sheria za uchaguzi na wajiepushe na matamshi yanayochochea vurugu na kuhatarisha usalama wa wananchi.
“Wanasiasa wafuate sheria na kanuni za uchaguzi zinavyosema tuepuke matamshi ambayo mtu wa kawaida akiyasikia hayatamuingiza katika kufanya vurugu,” alisema Msemaji wa Jeshi la Polisi Tanzania.
Amehimiza wananchi waepuke matumizi mabaya ya teknolojia hasa Akili Unde (AI) kwa kuwa imekuja kuwasaidia katika maisha na si kuvunja sheria, amani na usalama.
“Amani ikivurugika sio Polisi tu ataathirika, hata wewe uliyetengeneza utakuwa unakimbia kimbia, tujifunze kwa nchi nyingine nini kilichotokea na kinachoendelea. Tusiige vitu vinavyotoka nje ya mipaka yetu na kuvileta ndani ya nchi yetu, Watanzania tuna utamaduni wetu, tuna tunu zetu, tuzilinde,” alibainisha Misime.
Misime alisema Jeshi la Polisi limejipanga kuhakikisha Uchaguzi Mkuu unafanyika katika mazingira ya amani, utulivu na usalama.
Alisema jeshi hilo linatekeleza majukumu kwa kuzingatia maelekezo ya sheria na haliwezi kukamata watu kama hawahatarishi amani.
“Polisi hawawezi kwenda mahali popote pale akamkamate mtu au kuzuia kitu chochote kama haoni kuna uvunjifu wa sheria, wananchi wawe na amani, sisi tupo kusimamia jukumu lililo mbele yetu kwa kufuata sheria za nchi kama zinavyoelekeza,” aliongeza Misime.
Alisema polisi wanaendelea kufuatilia na kukamata wanaotengeneza taarifa za uongo na upotoshaji na kuendelea kutoa elimu kwa maofisa wa jeshi namna ya kuwadhibiti.
Alihimiza wananchi waendelee kutoa ushirikiano kwa polisi ili kulinda amani na wajiepushe na vurugu.
Alisema wamejipanga kusimamia sheria kwa weledi na halitasita kuwawajibisha watakaokiuka sheria kwa kuwafikisha mbele ya vyombo vya sheria ushahidi utakapokamilika.



