Polisi yaonya wanaofunika ushahidi

GEITA – JESHI la Polisi Nchini, Kamisheni ya Polisi Jamii limewataka wakazi wa Geita kuacha tabia ya kuficha ushahidi pale watuhumiwa wanapokamatwa kwani wanarudisha nyuma juhudi za kudhibiti uharifu.

Ofisa wa Kamisheni ya Polisi Jamii, Kamishina Msaidizi wa Polisi (ACP) Elisante Ulomi alitoa angalizo hilo kwenye mkutano wa hadhara na wakazi wa kijiji cha Nyawilimilwa, Halmashauri ya wilaya Geita.

Mkutano huo ni mwendelezo wa Kampeni ya siku 14 ya Kufikisha Elimu ya Ulinzi Shirikishi mkoani Geita iliyoratibiwa na Jeshi la Polisi kwa Ushirikiano na Kampuni ya Mgodi wa Dhahabu ya Geita (GGML).

Alisema bado kuna mwitikio mdogo kwa wananchi ikiwemo wakazi wa Geita kutoa ushahidi wa matukio ya uharifu, ukatili na unyanyasaji hali inayopelekea watuhumiwa wanaoshikiliwa kutotiwa hatiani.

ACP Ulomi amesema dhamira ya jeshi la polisi ni kulinda amani kwa kudhibiti watu wanaohatarisha usalama katika jamii lakini tabia ya kuficha ushahidi ni kiashiria cha usaliti na kuwalinda waharifu.

“Ndugu zangu tushirikiane, ile tabia ya kuoneana muhali huyu ni mtoto wa fulani, mtoto wa mjomba, hapana, uharifu tukitaka kuuzuzia na kuukomesha lazima tufike mahali tutoe ushahidi mahakamani”, amesema.

Mrakibu wa Polisi kutoka Kamisheni ya Polisi Jamii Makao Makuu Dodoma, Dk Ezekiel Kyogo amesema kila mtu ana nafasi ya kudhibiti uharifu kwa kufichua ama kuripoti mipango ya waharifu.

SOMA PIA: Polisi yaanza oparesheni watoto wa mitaani Geita

Amesema ili kudhibiti vitendo vya ukatili na uharifu ni lazima jamii iwe tayari kushirikiana na kubadilishana taarifa na jeshi la polisi kufanikisha adhima ya kubaini na kuzuia matukio hayo katika jamii.

“Mkituambia hayo mapema uharifu hautatokea, na kama hautatokea maana yake hatutatumia gharama kubwa kudhibiti na kuwasaka waharifu”, alisema Dk Kyogo.

Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Wilfred Willa amekiri wazazi na walezi wengi hawajitokezi kuandika maelezo pale wanapohitajika kutoa ushirikiano yanapotokea matukio ya ukatili wa kijinsia dhidi ya watoto wao.

“Niwaombe sana, suala la ukatili wa kijinsia, suala la kubaka, kulawiti, mashambulio ya aibu na vipigo visiishie nyumbani, visiishie ofisi ya kata, hapana, pelekeni polisi, na haliishii hapo, litaiishia mahakamani”, amesema.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button