PURA yaipongeza TPDC gesi asilia katika uchumi

DAR ES SALAAM: MKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA), Mhandisi Charles Sangweni, amesema kugundulika kwa gesi asilia nchini kumeleta manufaa makubwa kwa wananchi, hasa katika sekta za kilimo, ufugaji, usafirishaji na matumizi ya nyumbani, na hivyo kuchochea ukuaji wa uchumi wa taifa kwa ujumla.

Sangweni mmesema hayo jana Agosti7,2025 alipotembelea banda la Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) katika Maonesho ya Nane Nane yanayoendelea jijini Dodoma, na kujionea teknolojia mbalimbali za usimamizi na usambazaji wa gesi asilia zinazotekelezwa na TPDC kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini.

“Gesi asilia, ambayo kimsingi ni Methane (CH₄), inachangia uzalishaji wa mbolea ya Ammonium Sulphate au Ammonium Phosphate kupitia kiwanda maalum kinachotenganisha na kutengeneza Ammonium. Mbolea hii ni muhimu katika kuongeza tija mashambani,” amefafanua.

Aidha, Mhandisi Sangweni amesema kuwa matumizi ya gesi kwenye vyombo vya moto yana faida kubwa kwani husaidia kupunguza gharama za matengenezo kutokana na ufanisi wake wa kiufundi.

“Mfumo wa gesi unapunguza hitaji la kutumia mafuta ya petroli mara kwa mara, na hivyo huchochea muda mrefu wa huduma kwa vifaa kama vile fuel pump, filters na hata spark plugs; ambazo hazichafuki kwa haraka,” amesema

Amezisifu jitihada za TPDC katika kupanua miundombinu ya gesi nchini, ikiwemo ujenzi wa mtandao wa usambazaji gesi asilia jijini Dodoma pamoja na uwepo wa vituo vya gesi vya muda (mobile gas stations) katika jiji hilo.

“Kwa kutumia gesi, gari linaweza kusafiri zaidi ya kilomita 40 kwa kiasi kilekile cha mafuta ambacho kingesafiri kilomita 10 tu kwa petroli. Kwa bajaji, unaweza kwenda zaidi ya kilomita 60 badala ya 30. Huu ni unafuu mkubwa kwa wananchi,” alisisitiza.

Mtaalamu huyo kutoka PURA alihamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika matumizi ya gesi kwa shughuli za kupikia na usafiri ili kuokoa gharama, kulinda mazingira na kuongeza kasi ya maendeleo ya kiuchumi.

Ameupongeza uongozi wa wizara ya nishati chini ya Naibu Waziri Mkuu, Dk Doto Biteko, Bodi ya TPDC na Serikali kwa ujumla kwa kuendeleza usimamizi madhubuti wa sekta ya gesi nchini.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button