Raila Odinga kuzikwa keshokutwa

KAMATI ya Mazishi ya Kiongozi wa Upinzani nchini Kenya, Raila Odinga imesema kiongozi huyo atazikwa Jumapili, Oktoba 19 kulingana na matakwa ya familia yake.

Raila alifariki dunia juzi nchini India alikokuwa akipatiwa matibabu.

Akizungumza na wanahabari mjini Nairobi, Naibu Rais, Profesa Kithure Kindiki alisema kiongozi huyo mkongwe katika siasa za Kenya, aliweka wazi kwa familia yake kuwa atakapoaga dunia, azikwe ndani ya saa 72 baada ya kifo chake.

Profesa Kindiki alisema Raila ataandaliwa mazishi ya kitaifa kwa heshima kamili ya dola.

Jiji la Nairobi lasimama

Maelfu ya wananchi wa Kenya, wakiongozwa na Rais Dk William Ruto walijitokeza kwenye Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Jomo Kenyatta (JKIA) kuupokea mwili wa Raila na kusababisha shughuli zote katika jiji hilo kusimama kwa muda kupisha msafara huo.

Mabomu ya machozi yarindima

Polisi Mjini Nairobi wametumia gesi na mabomu ya kutoa machozi kuwatawanya waombolezaji waliokusanyika katika Uwanja wa mpira wa Kasarani, baada ya kutokea msongamano mkubwa wa watu waliojitokeza kutaka kuuaga mwili wa Raila.

Ratiba ya bungeni yabadilishwa

Ratiba ya kupeleka mwili wa Raila katika Viwanja vya Bunge kwa ajili ya kuwapa fursa wabunge kumuaga ilibadilishwa ghafla, kutokana vurugu kubwa baada ya waombolezaji kutaka kuingia ndani ya bunge.

Ingawa mwili wa Raila ulikuwa haujafika katika viwanja vya bunge, wananchi hao walitaka kuingia ndani na kukaa wakiusubiri.

Hata hivyo, polisi ililazimika kutumia nguvu baada ya waandamanaji waliokuwa wamekusanyika pembeni ya Barabara ya Bunge, walipovunja vizuizi vya njia hiyo na kuviweka kando ya Barabara ya City Hall.

Kaka wa Odinga ateuliwa kuongoza ODM

Seneta wa Siaya, Oburu Odinga ameteuliwa kuwa kaimu kiongozi wa Chama cha Orange Democratic Movement (ODM) kuchukua nafasi ya mdogo wake Raila aliyefariki juzi nchini India alikokuwa akipokea matibabu.

Kiwanja cha Ndege JKIC chafungwa kwa muda

Mamlaka ya Usafiri wa Anga nchini Kenya (KCAA) ililazimika kusitisha kwa muda shughuli zote katika JKIA, kutokana na taharuki iliyoibuka baada ya kuwasili kwa mwili wa Raila.

Katika taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana, KCAA ilisema kundi kubwa la waombolezaji lilivamia maeneo ya uwanja yaliyokuwa yamewekewa vizuizi vya kiusalama, hatua iliyolazimu uwanja kufungwa kwa tahadhari ili kutoa nafasi kwa vikosi vya usalama kurejesha utulivu na kuhakikisha usalama wa wasafiri na wafanyakazi wa uwanja huo.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button