Rais atangaza Baraza la Mawaziri la kimkakati

RAIS Samia Suluhu Hassan ametangaza Baraza la Mawaziri la kimkakati lenye wizara 27 huku kukiwa na mabadiliko kadhaa ikilinganishwa na lililomaliza muda wake.

Ameanzisha Wizara ya Maendeleo ya Vijana ambayo alifafanua kwamba ni baada ya kuona umuhimu wa uwepo wake na itakuwa chini ya Ofisi ya Rais.

Pia, amesema amefanya marekebisho kidogo kwenye Wizara ya Kazi, Ajira na Vijana na kuondoa vijana hivyo kuanzisha Wizara ya Kazi, Ajira na Mahusiano.

SOMA: Rais Samia ateua Mawaziri 27, Naibu Mawaziri 29

“Maana yake ni kwamba atakayeshika wizara hii ya mahusiano atakuwa na kazi kubwa ya kufanya mazungumzo na makundi na wahusika mbalimbali nchini kwa ajili ya kujenga mahusiano mazuri, na wizara hii itakuwa chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu,” amesema Samia.

Aidha, ameihamisha Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kutoka Ofisi ya Rais na kuirudisha Ofisi ya Waziri Mkuu kama ilivyokuwa awali.

Katika baraza hilo, mawaziri 18 waliokuwa katika lililopita, wameteuliwa na kuingia katika baraza la sasa. Sura mpya kwa maana ya ambao hawakuwa katika baraza lililopita, ni tisa.

Aidha, naibu mawaziri wanane waliokuwa katika baraza lililopita, wameteuliwa katika baraza jipya lililotangazwa jana na Rais Samia Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma na waliobaki ni wapya katika nafasi hiyo.

Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambayo inaongozwa na Profesa Palamagamba Kabudi, sasa ina naibu mawaziri wawili tofauti na baraza lililopita ambalo alikuwa mmoja.

Mawaziri saba waliokuwa katika baraza lililopita ambao hawakuingia baraza jipya ni Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko, Hussein Bashe (Kilimo), Innocent Bashungwa (Mambo ya Ndani), Jenista Mhagama (Afya), Dk Seleman Jafo (Viwanda na Biashara), Dk Pindi Chana (Maliasili na Utalii) na Dk Damas Ndumbaro (Katiba na Sheria).

Kati ya mawaziri wateule, watano ni ambao waliteuliwa ubunge na Rais Samia Novemba 10, 2025. Nao ni Dk Dorothy Gwajima (Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu) huku naibu wake akiwa Maryprisca Mahundi.

Mwingine ni Balozi Khamis Mussa Omar (Wizara ya Fedha) ambaye wizara yake ina manaibu wawili ambao ni Laurent Luswetula na Mshamu Ali Munde. Balozi Mahmoud Thabit Kombo ameteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na atakuwa na manaibu wawili ambao ni Dk Ngwaru Maghembe na James Millya.

Wabunge wengine wa kuteuliwa ni Dk Rhimo Nyansaho ambaye ameteuliwa kuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa na Dk Bashiru Ally ambaye ameteuliwa kuwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi na naibu wake akiwa Ng’wasi Kamani.

Aidha, waliokuwa naibu mawaziri katika baraza lililopita ambao wameteuliwa kuwa mawaziri ni aliyekuwa Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga ambaye sasa amekuwa Waziri wa Viwanda na Biashara.

Kwa upande wake, aliyekuwa Naibu Waziri Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Deus Sangu ameteuliwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano na naibu wake akiwa Rahma Riadh Kisuo.

Mawaziri wapya ni Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo na Mbunge wa Lushoto, Profesa Riziki Shemdoe aliyeteuliwa kuwa Waziri katika Ofisi ya Waziri Mkuu Tamisemi.

Awali amekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi. Mbunge wa Mtwara Mjini, Dk Joel Nanauka ameteuliwa kuwa Waziri, Ofisi ya Rais Maendeleo ya Vijana.

Uapisho wa mawaziri na naibu mawaziri wateule utafanyika Ikulu Chamwino Dodoma leo.

 

Habari Zifananazo

2 Comments

  1. I get paid over (90$ to 500$ / hour ) working from home with 2 kids at home. I never thought I would be able to do it but my best friend earns over $22000 a month doing this and she convinced me to try. it was all true and has totally changed my life… This is what I do, check it out by Visiting Following web….
    .
    HERE——————————————⊃⫸ http://Www.Cash43.Com

  2. Google is now paying $300 to $500 per hour for doing work online work from home. Last paycheck of me said that $20537 from this easy and simple job. Its amazing and earns are awesome. No boss, full time freedom and earnings are in front of you. This job is just awesome. Every person can makes income online with google easily……….
    .
    M­­­­­­o­­­­­­r­­­­­­e­ D­­­­­­e­­­­­­t­­­­­­a­­­­­­i­­­­­­l­­­­­­s For Us→→→→→→→→→→ http://Www.Payathome9.Com

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button