Rais Chakwera akubali kushindwa uchaguzi

MALAWI : RAIS wa Malawi, Lazarus Chakwera, amekubali kushindwa uchaguzi mkuu na kuliambia taifa lake kwamba anafanya hivyo kwa kuheshimu matakwa yao ya mabadiliko ya serikali.

Akihutubia taifa kabla ya kutangazwa rasmi kwa matokeo leo mchana, Chakwera alitambua matokeo ya awali yaliyoonyesha mpinzani wake, Rais wa zamani Peter Mutharika, anaongoza kwa karibu asilimia 66 ya kura zilizohesabiwa kufikia Jumanne, huku yeye akipata 24%.

“Ninajua kwamba kwa wengi wenu mliopiga kura, matokeo haya ni taswira ya nia yenu ya pamoja ya kuwa na mabadiliko ya serikali na hivyo ni sawa kukubali kushindwa kutokana na kuheshimu matakwa yenu kama raia,” alisema Chakwera.

Rais huyo pia alithibitisha kuwa amempigia simu Mutharika kumpongeza kwa “ushindi wake wa kihistoria” na kuahidi kuunga mkono mchakato wa amani na usalama katika taifa hilo. Chakwera aliongeza kwamba alifika mahakamani jana kujaribu kuzuia kutangazwa kwa matokeo, lakini anakubali uamuzi wa mahakama kwamba tume ya uchaguzi iendelee na kutangaza matokeo rasmi.

“Wamalawi, kama mko upande wa kushindwa au kushinda, tafadhali muwe na amani,” aliwasihi wananchi. SOMA: MCP yadai kuibiwa kura uchaguzi Malawi

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button