Rais Samia akemea ramli chonganishi

ZANZIBAR;  RAIS Samia Suluhu Hassan amewataka viongozi wa dini kuitumia nafasi yao vizuri kwa ajili ya kuwajengea imani wafuasi wao kuachana na tabia ya kupenda kupiga ramli chonganishi ambayo ni chanzo
cha fitina na mivutano na kusababisha migogoro katika jamii na familia.

Samia alisema hayo wakati akizungumza katika kongamano la wanawake wa Kiislamu katika kuadhimisha mwaka mpya wa Kiislamu wa 2446 hijria mjini Unguja, Zanzibar.

Alisema matibabu ya tiba asili yanafahamika lakini yanatakiwa kuratibiwa vizuri na kujiepusha kupiga ramli ambayo husababisha kuwepo kwa imani potofu.

Alisema hivi sasa familia nyingi zimeingia katika migogoro na kutuhumiana katika masuala ya uchawi
na ushirikina kutokana na kujishughulisha na kupiga ramli chonganishi ambayo ndiyo sababu ya chuki na
uhasama.

Alisema jamii inapoamini masuala ya ushirikina kwa kiasi kikubwa maana yake inaondoka katika mstari
wa kumuamini Mwenyezi Mungu kwamba ndiye mola muumba wa kila kitu.

“Huko jamani hatutakiwi kufika….viongozi wa dini tuwajenge vizuri imani wafuasi wetu kurudi katika imani na kumcha Mungu na kuamini kwamba kila kitu uwezo wake ni kudra ya Mwenyezi Mungu,” alisema.

Aidha, aliwataka viongozi ikiwemo wanasiasa kujenga tabia ya kuwa na ndimi laini za tabia nzuri na kutamka
maneno ya hekima na busara  ikiwemo kuyatumia vizuri majukwaa ya kisiasa.

Isome pia:https://habarileo.co.tz/chalamila-siwaogopi-waganga-wa-kienyeji-nitawasafisha-dar/

Aliwaonya wanasiasa kuyatumia vizuri majukwaa ya kisiasa ambayo kwa kawaida huwa na hamasa kali
na jazba na hisia za maneno yanayotishia uvunjifu wa amani na utulivu.

Alisema kuwepo kwa amani na utulivu ndiyo nafasi nzuri kwa serikali kufanya shughuli zake za kuwatumikia na kuwaletea wananchi maendeleo.

Alitoa hadithi ya Imamu Buhari na Muslim ambayo inasisitiza kiongozi aliyechaguliwa kuongoza kwa kiasi
kikubwa anatakiwa kutumia busara na hekima katika kuwaongoza wafuasi wake.

Aliyataja baadhi ya maadili kwa viongozi waliochaguliwa kuwa na kauli zilizonyooka pamoja na weledi
katika kutatua changamoto zinazowakabili wananchi.

“Kiongozi ni sawa na mti wenye kivuli unatakiwa kujiamini pamoja na kuongoza kwa kutumia busara na
hekima kiasi ya kujenga tabia ya kuaminika,” alisema.

Awali, alisisitiza umuhimu wa kulipa kodi ambayo limezungumzwa katika moja ya mada iliyowasilishwa katika
kongamano hilo.

Alisema hakuna serikali inayoongozwa duniani bila ya wananchi kulipa kodi, kutoa fursa ya kufanyika kwa
shughuli za maendeleo.

Isome pia:https://habarileo.co.tz/imani-za-kishirikiana-ni-janga-nyanghwale/

Kwa mfano alisema serikali inapata nguvu ya kufanya mambo yake kwa maslahi ya wananchi
kwa ajili ya kukusanya kodi katika maeneo muhimu ikiwemo kwa wafanyabiashara wadogowadogo kuhalalisha shughuli zao kisheria.

Alisema miongoni mwa mambo yanayomkereketa na kumuumiza kichwa ni tatizo la wananchi na wafanyabiashara kushindwa kulipa kodi ambapo hata hivyo juhudi zinazochukuliwa zimeanza kuonesha muelekeo ikiwemo wa kuongezeka kwa mapato ya makusanyo ya kodi.

Alisema kwa upande wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano imefanikiwa kupandisha mapato yanayotokana na kodi kutoka Sh trilioni 24.1 katika mwaka 2022/2023 hadi kufikia Sh trilioni 27.63 katika mwaka 2023/2024.

“Serikali haina miujiza katika kuendesha shughuli zake isipokuwa inategemea kodi tumefanikiwa kwa
kiasi kikubwa kufuatia kutumia ulimi laini pamoja na utawala bora na sheria katika kukusanya kodi,”
alisema.

Isome pia:https://habarileo.co.tz/lambalamba-170-mbaroni-ramli-chonganishi/

Aidha, aliwaambia wanawake kwamba wametukuzwa katika kitabu kitukufu cha Kurani na kutajwa katika daraja la juu kutokana na kukabiliwa na majukumu ikiwemo kutunza familia na nyumba.

Alizitaja Suratul Luqman pamoja na Suratul Al-qasas ambazo zote zinataja daraja la mwanamke katika kutukuzwa
na Mwenyezi Mungu huku akipewa heshima kubwa ikiwemo ya kubeba ujauzito miezi tisa na kunyonyesha miaka miwili.

Aliwataka viongozi wa dini kuzitumia hotuba za swala ya Ijumaa kuyaelezea mambo ya utukufu na daraja
aliyopewa mwanamke badala  ya kuchukua muda mwingi kwa ajili ya kuzitaja kasoro zao.

Habari Zifananazo

Back to top button