Rais Samia azindua mradi wa kuchenjua urani Namtumbo

RUVUMA: RAIS  Samia Suluhu Hassan leo Julai 30, 2025 amezindua Kiwanda cha majaribio cha kuchenjua Urani wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma, ukiwa ndiyo mradi mkubwa na wa pekee wa urani kwa ukanda wa Afrika Mashariki.

Mradi huo umejengwa katika eneo la Mkuju River wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma, ukitarajiwa kuwa chachu ya mageuzi makubwa ya kiuchumi, kitaalamu na Kidiplomasia katika Ukanda wa Afrika Mashariki, Mradi ukitarajiwa kuanza rasmi mwaka 2026 na kugharimu zaidi ya Sh trilioni 3.06, ukitarajiwa pia kuwa sehemu ya uzalishaji wa nishati ya umeme nchini.

Mantra Tanzania Limited ndiyo kampuni kuu inayosimamia mradi huo ikishirikiana na makampuni ya kimataifa kama Rosatom ya Urusi kwa uendelezaji wa miundombinu na teknolojia, mradi ukitarajiwa pia kujenga uwezo kwa wazawa kwani uvunaji wa urani ni sekta mpya ya uchimbaji nchini Tanzania.

Kulingana na Wizara ya Madini nchini Tanzania, tafiti mbalimbali zilizofanyika zimeonesha madini ya Urani nchini Tanzania yaligundulika katika maeneo mbalimbali ikiwemo eneo la Namtumbo (Mkuju River), Bahi, Galapo, Minjingu, Mbulu, Simanjiro, Ziwa Natroni, Manyoni, Songea ,Tunduru, Madaba pamoja na Nachingwea Mkoani Lindi.

Tanzania itakapoanza uzalishaji kupitia Mradi wa Mkuju River Wilayani Namtumbo itakuwa nchi ya tatu barani Afrika kwa uzalishaji wa madini ya urani baada ya nchi ya Niger yenye akiba ya tani 200,000 na Namibia yenye akiba ya tani 100,000 katika miradi yake mitatu ya uzalishaji. Nchi ya Niger ndiyo nchi inayoongoza kwa uzalishaji wa urani barani Afrika na ni miongoni mwa wazalishaji wakuu duniani.

Uzalishaji wake unafanyika katika migodi mikubwa miwili ambayo ni Arlitna na Akouta inayomilikiwa na kampuni ya Kifaransa ya Orano zamani ilijulikana kama Areva.

Nchi ya Namibia pia ni mzalishaji mkubwa wa urani kupitia migodi yake maarufu ya Rossing Mine inayomilikiwa na Rio Tinto kwa kushirikiana na serikali ya Namibia pamoja na Husab Mine inayomilikiwa na kampuni ya Kichina.

Madini ya urani hutumika katika sehemu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuzalisha nishati ya umeme, matibabu na viwandani kwaajili ya kutengeneza rangi na glasi kutokana na uwezo wa madini hayo katika kutoa mionzi.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button