RAS Arusha ataka mikopo ikusanywe iwafaidishe wengine

ARUSHA: KATIBU Tawala Mkoa wa Arusha, Missaile Musa ameitaka Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro kuhakikisha inakusanya fedha za mikopo ya 10% inayotolewa na serikali kupitia wanawake, vijana na makundi maalum ili kuwezesha mikopo mingine kutolewa.
Aidha, hoja zinazozalishwa zijibiwe kwa wakati ili kuondoa mkanganyiko kutoka kwa Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) ikiwemo kuzipunguza zaidi
Ras Missaile ameyasema hayo jana wilayani Ngorongoro wakati wa mapitio ya hoja za ukaguzi kwa mwaka 2023/24 ambapo halmashauri hiyo imepata hati safi
Amesema ni vema madeni ya wazabubi na wakandarasi yalipwe kwa wakati ili kuondoa malalamiko kwa watoa huduma hizo ikiwemo hoja za ukaguzi.

Naye, Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Kanali, Wilson Sakulo alikiri mikopo ya asilimia kumi bado ina changamoto ya urejeshwaji wake lakini watashirikiana na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Mutual Mbillu kuhahakikisha fedha hizo zinarejeshwa kwa wakati ili kuwezesha makundi hayo kuendelea kupata mikopo
“Naomba mnaokopa mikopo turejeshe kwa wakati haiwezekani serikali itoe Sh milioni 520 kwa ajili ya mikopo hiyo halafu marejesho yake yasuesue hapana mnaokopa mikopo rejesheni kwa wakati,” amesema.
Wakati huo huo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ngorongoro, Murtalla Mbilu amesema halmashauri hiyo imepata hati safi huku ikiwa na hoja chache ikiwemo kuzuia uzembe na ubadhirifu ikiwemo ushirikiano baina yao na wakaguzi.




