RC Kheri James: Iringa tumejipanga ulinzi uchaguzi mkuu

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, amesema mkoa huo umejipanga ipasavyo kuhakikisha amani, utulivu na usalama vinatawala siku ya kupiga kura Oktoba 29 mwaka huu, ili wananchi waweze kutekeleza haki yao ya kikatiba kwa utulivu, uhuru na bila hofu.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake leo RC James alisema vyombo vya ulinzi na usalama vimeweka mikakati madhubuti kuhakikisha uchaguzi unafanyika katika mazingira salama na tulivu, hivyo kuwataka wananchi wote kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura.

“Nawasihi wananchi wote wa Iringa wajitokeze kwa wingi kupiga kura. Tumejipanga kuhakikisha kila mtu anatekeleza wajibu wake bila wasiwasi wowote. Hakutakuwa na vitisho, vurugu wala usumbufu,” alisema RC James.

Amesema vyombo vya ulinzi na usalama vipo katika kila eneo kuhakikisha hakuna mtu au kikundi kinachoweza kuvuruga utulivu wa uchaguzi, na huduma zote muhimu za kijamii zitaendelea kutolewa kama kawaida.

“Pamoja na kupiga kura wananchi waendelee na shughuli zao bila hofu. Serikali inawahakikishia hali ya usalama ni shwari. Hatutakubali mtu yeyote au kikundi chochote kuvuruga amani iliyopo,” alionya.

RC James pia ametoa wito kwa wananchi kuendeleza umoja na mshikamano, akisisitiza kuwa uchaguzi ni sehemu ya mchakato wa kidemokrasia, hivyo unapaswa kuendeshwa kwa amani na kuheshimiana.

“Tujitokeze kupiga kura kwa amani, tuwe na uvumilivu na tuilinde heshima ya mkoa wetu. Vyombo vya ulinzi na usalama vipo imara, makini na tayari kuchukua hatua dhidi ya yeyote atakayejihusisha na vitendo vya uvunjifu wa amani,” alisema kwa msisitizo.

Habari Zifananazo

One Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button