RC Mtwara ahimiza wananchi kujitokeza msaada wa kisheria

MKUU wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Patrick Sawala amewataka wananchi mkoani humo kujitokeza kwa wingi kupata elimu na huduma ya msaada wa kisheria kupitia kampeni ya msaada wa Kisheria ya Mama Samia iliyozinduliwa rasmi mkoani humo.

Akizungumza mkoani Mtwara alipozindua kampeni hiyo ya msaada wa Kisheria ya Mama Samia (Samia Legal Aid) Mtwara uliyofanyika katika Manispaa ya Mtwara Mikindani, mkuu huyo wa mkoa amesema kampeni hiyo imekuwa mkombozi mkubwa kwa wanyonge wasioweza kumudu gharama za mawakili pia imepunguza mlundikano wa mashauri mahakamani.

Advertisement

Aidha lengo la kampeni hiyo ikiwa ni pamoja na kutoa elimu na kutatua changamoto mbalimbali za kisheria zinazowakabili wananchi mkoani humo hususani katika masuala ya mirathi, migogoro ya ardhi, ukatili wa kijinsia, masuala ya ndoa na mengine.

‘’Kampeni hii ya msaada wa kisheria itasaidia watu wetu kujua haki zao, mtu akiwa na haki yake ameipata kihalali atakuwa na amani na hii itaimarisha utulivu na usalama katika mkoa wetu na hivyo watu wetu wataweza wakafanya shughuli zao za kimaendeleo bila kubugudhiwa,’’amesema Sawala.

Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Kisheria kwa Umma kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Abdurahmani Mshamu amebainisha baadhi ya huduma zitakazo tolewa ikiwa pamoja na elimu ya usimamizi wa mirathi na urithi na kusema kuwa kampeni hiyo itafanyika kwa muda wa siku kumi mkoani humo.

Naye Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara, Rose Ibrahim amesema kampeni hiyo inaendelea kutoa elimu kuhusu msaada wa kisheria kwa wananchi na inatarajiwa kuwa na manufaa makubwa katika jamii ya Mtwara.

Baadhi ya wananchi mkoani humo akiwemo Diana Chacha mkazi wa magomeni katika manispaa hiyo, ameishukuru serikali kwa kuanzisha kampeni hiyo ambayo kwa kiasi kikubwa inakweda kutatua changamoto mbalimbali za kisheria zinazo wakabili wananchi.