RC Mtwara akagua miradi ya maendeleo Mtwara

MKUU wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Patrick Sawala amefanya ziara ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo akiambatana na baadhi ya viongozi wa vyama mbalimbali vya siasa vilivyopo mkoani Mtwara.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo iliyofanyika leo Novemba 18, 2024, Mkuu huyo wa Mkoa amesema lengo la ziara hiyo ni kuwaonyesha viongozi hao wa vyama vya siasa jitihada zinazofanywa na serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Aidha serikali imewekeza kwenye miradi mbalimbali ya maendeleo katika mkoa huo ikiwemo maboresho kwenye Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) yaliyogharimu zaidi ya kiasi cha Sh bilioni 157.8 na kuwezesha bandari kufanya kazi kwa ufanisi zaidi.

Advertisement

Akizungumza kwa niaba ya viongozi wengine wa siasa Katibu wa Chama cha Wananchi (CUF) Jimbo la Mtwara Mjini Said Kulaga, amempongeza Mkuu huyo wa Mkoa kwa kuwashirikisha viongozi hao wa vyama vya siasa kwa ajili ya kufahamu kile kinachofanyika katika bandari hiyo ambayo imewekezwa kiasi kikubwa cha fedha.

“Nitoe wito kwa viongozi wengine kuiga mfano wa RC Sawala kwa kuwashirikisha viongozi wa vyama pinzani ili kusukuma kwa pamoja gurudumu la maendeleo katika mkoa wetu na naomba isiwe tu katika kipindi cha kuelekea kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27, 2024 bali liwe zoezi endelevu”amesema Kulaga

Meneja wa Bandari ya Mtwara, Ferdinand Nyathi amesema bandari hiyo ina ufanisi mkubwa wa kutoa huduma mbalimbali na mpaka tayari sasa wameshahudumia zaidi ya tani elfu 79,000 za korosho ghafi kwa msimu huu wa korosho mwaka 2024/2025.

Aidha, mpaka sasa meli nne zilizobeba korosho ghafi zimeshaondoka bandarini hapo kuelekea nje ya nchi hususani India pamoja Vietnam.

Hata hivyo amezungumzia ujenzi wa gati mpya unaotarajiwa kujengwa katika kisiwa mgao kuwa, serikali ina nia thabiti kwa ajili ya kuongeza maeneo ya kuhudumia shehena katika bandari hiyo na wananchi kunufaika kutokana na uwepo wa bandari.