RC Tanga ataka uchaguzi mitaa uwe 100 %

MKUU wa Mkoa wa Tanga, Dk Batilda Burian amewahimiza wakuu wa wilaya na wasimamizi wa uchaguzi mkoani humo kuhakikisha upigaji kura katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa Novemba 27, mwaka huu unafikia asilimia 100.

Dk Batilda ameyasema hayo leo na Dk Batilda alipofanya ziara ya kukagua maandalizi ya uchaguzi huo katika halmashauri za wilaya na mji Handeni, akiongozana na Katibu Tawala Mkoa, Pili Mnyema, Kamati ya Usalama (KU) na Kamati ya Uratibu wa Uchaguzi mkoani humo.

Advertisement

Amesema mafanikio yaliyofikiwa kuandikisha asilimia 110.82 ya wapiga kura na kushika nafasi ya pili kitaifa, yamepongezwa na Rais Samia Suluhu Hassan, hivyo kuibua haja ya kuhakikisha watu wote wanapiga kura.

‘’Tumefanikiwa kuandikisha wapiga kura kwa asilimia 110.82 kwa zoezi lililofanyika kwa siku 10, sasa tuna saa 10 tu kwa siku moja, kuhakikisha kila aliyejiandikisha anapiga kura ili tuuheshimishe uchaguzi huo na kumheshimisha Mhe Rais Samia Suluhu Hassan,’’ amesema.

Aliwakumbusha wasimamizi wa uchaguzi kufuata sheria, kanuni na taratibu zilizopo, ili uchaguzi huo ufanyike na kuthibitika pasipo shaka kuwa ni wa wazi, huru na haki.

Naye Katibu Tawala Mkoa, Pili Mnyema amesema pamoja na mafanikio yanayoonekana kwenye taarifa za halmashauri hizo, Mkuu wa Mkoa na timu zake, anafanya ziara hizo ili kujiridhisha na uhalisia uliopo, kisha kusaidia utatuzi wa changamoto zinazojitokeza.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Albert Msando, amesema maandalizi ya uchaguzi huo vikiwemo vifaa vitakavyotumika, yamefikia hatua nzuri, hivyo kuwa na uhakika wa kufanyika kwa uchaguzi huru, wazi na haki.