MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA), Mkoa wa Morogoro imewataka wataalamu kutoka idara na taasisi za serikali mkoani humo kuhakiki risiti kabla ya kufanya malipo kwa wazabuni na wakandarasi wanaojihusisha na miradi mbalimbali ya ujenzi.
Hatua hiyo itawasaidia kubaini risiti bandia na kuwachukulia hatua stahiki kwa watakaobainika kuandaa risiti bandia.
Meneja msaidizi wa huduma kwa walipa kodi mkoa huo, Chacha Gotora amesema hayo wakati wa utoaji elimu ya kodi kwa wataalamu kutoka idara na taasisi za serikali zilizopo ndani ya mkoa huo.
Amesema lengo la kutolewa elimu hiyo ni kuwepo kwa changamoto katika taasisi za umma kwenye kuhakiki risiti kwa vile imeonekana kuna wimbi la kupelekewa risiti ambazo si sahihi pindi wanapofanya manunuzi.
Corota ametaja eneo lingine ni kuwapa uelewa wa namna ya kuhakiki risiti za kieletroniki ili kuweza kujua risiti ipi ni sahihi na ni vitugani vilivyomo kwenye risiti hizo na ipi si risiti sahihi.
Amesema baada ya kugundua changamoto hiyo TRA mkoa iliamua kuwakutanisha wataalamu hao na kuwapa elimu hiyo ikiwa na kuwaelekeza umuhimu wa kuhakiki risiti kabla ya kufanya malipo kwa wazabuni na wakandarasi.
Cotora amesema hatua hiyo itasaidia kubaini zile risiti bandia na kuweza kuwachukulia hatua wale watakaobainika wanaziandaa risiti hizo.
“ Tumewakutanisha wakuu wa taasisi za umma ,wahasibu na maofisa ugavi wa taasisi za Serikali zilizopo mkoani Morogoro na hatua hii inatokana na kesi nyingi ambazo TRA ilikuwa inazipata kutoka kwenye Taasisi hizi,” amesema Cotora.
Pia amesema elimu hiyo ilihusisha masuala ya ulipaji na ukataji wa kodi ya zuio kwa taasisi za umma, kutekeleza wajibu wao wa namna ya kulipa kodi na kujadili masuala ya kodi ili wawe na uelewa mpana zaidi wakati wa kutekeleza majukumu yao ya kikazi.
Cotora amesema elimu imetolewa kwao kuhusu namna ya uombaji wa misamaha kwenye kodi ya ongezeko la thamani kwenye miradi inayowekezwa na taasisi za serikali, namna ya kudai risiti wanapofanya manunuzi na kutoa risiti kwa zile taasisi za kiserikali ambazo zinatumia mifumo ya kodi nchini.
Nao baadhi ya washiriki akiwemo mlipakodi ,Deogratius George amesema huwa wanakabiriwa na changamoto katika malipo ya serikali .
George amesema taratibu za TRA inataka kuwa zinapotolewa huduma kuwepo na risiti ,lakini kwa baadhi ya taasisi za serikali zinakosa uaminifu wa kulipa fedha kwa wakati .
“ Kitu kinachotokea tunakata risiti kabla , lakini baadhi ya taasisi hazina uaminifu wa kulipa kwa muda na nyingine hazilipi na tupotoa risiti kulingana na takwa la TRA inamaanisha tumeshalipwa fedha tayari wakati sio,” amesema George.