Rolinga apiga jeki wenye ulemavu

DAR ES SALAAM: KATIKA kuadhimisha siku yake ya kuzaliwa, Nabii Samwel Samson Rolinga, maarufu kama SS Rolinga, ametoa msaada wa viti mwendo zaidi ya 20 kwa watoto wenye ulemavu pamoja na kula chakula na wenye uhitaji maalumu.

Tukio hilo limefanyika katika ibada ya shukrani kwenye Kanisa la Omega Ministries Church of All Nations, Dar es Salaam jana.

Akiwa ameungana na waumini wake pamoja na wageni kutoka mikoa na mataifa mbalimbali kwenye ibada hiyo ya shukrani, Nabii Rolinga alisema ameona ashiriki katika kusaidia kundi hilo ili na wao waweze kwenda shule.

“Watoto hawa wanashindwa kwenda shule kwa sababu hawana viti mwendo, nimeona nitumie siku yangu kusema Asante Mungu lakini pia kuwasaidia wenye mahitaji kutimiza malengo yao ya kielimu,”amesema.

Alisema: “Naomba wazazi wasiwafiche watoto wenye ulemavu majumbani. Tuwaoneshe upendo kwa kuwapeleka shule. Hili ndilo agizo la Mungu – kusaidia na kuinua waliodharauliwa,” alisema Nabii Rolinga kwa msisitizo huku akiishukuru hospitali ya CCBRT kwa kufanikisha awamu ya kwanza ya viti hivyo. Pia, anatarajia kutoa miguu bandia kwa ajili ya makundi hayo.

 

Ibada hiyo ilihudhuriwa na makundi mbalimbali ya watu wenye mahitaji maalumu, ambapo walishiriki chakula cha pamoja kama ishara ya mshikamano, upendo na matumaini mapya.

Nabii Rolinga aliwahakikishia kuwa Kanisa lake litaendelea kuwa sehemu ya faraja kwa jamii zilizojeruhiwa kiakili, kimwili au kiroho.

Tukio hilo limeacha alama kubwa ya matumaini na faraja kwa watoto waliopokea msaada huo pamoja na familia zao, na kuonesha kwa vitendo kile kinachoitwa upendo wa dhati kwa walio katika mazingira magumu.

 

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button