Samia aacha ahadi 4 Nyanda za Juu Kusini
MGOMBEA wa urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan amefanya mikutano 11 ya kampeni katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini. Samia amefanya mikutano hiyo kuomba kura za wananchi katika mikoa ya Songwe, Mbeya, Njombe na Iringa.
Katika mikoa hiyo Samia ameahidi kuendeleza sekta ya kilimo, ujenzi wa viwanda, kuimarisha huduma za kijamii na kuinua wajasiriamali.
Katika sekta ya kilimo, Samia aliwahakikishia wakulima kuwa CCM ikiingia madarakani katika miaka mingine mitano, itaendelea kuwapatia wakulima mbolea ya ruzuku, viwatilifu na mbegu ili wakulima waendelee kulima kwa tija.
Amesisitiza serikali yake bado ina uwezo wa kutoa ruzuku kwenye pembejeo na kuwataka wakulima kuendelea kujisajili huku akiwaonya kutoshirikiana na watu waovu kuuza pembejeo za ruzuku.
Tangu kuanza kutolewa kwa mbolea ya ruzuku wakulima wamelima kwa tija na kwa mwaka huu Tanzania imeshika nafasi ya pili Afrika kwa kuzalisha mahindi tani milioni 10 na ukichanganya na mazao mengine kumeifanya nchi iwe na utoshelevu kwa chakula kwa asilimia 128.
Samia amewapongeza wakulima wote nchini kwa kuzalisha kwa tija na kuifanya Tanzania ifanye vizuri kwenye mauzo ya chakula nchi za nje.
SOMA: Samia na hotuba ya matumaini uzinduzi wa kampeni CCM
Pia, ameahidi kuimarisha kilimo cha chai katika mikoa ya Mbeya, Njombe na Iringa na kusisitiza serikali imeunda timu inayofanya tathmini ya kina kuhusu mashamba na viwanda vya chai kote nchi na endapo wawekezaji waliopo wataonesha kushindwa, serikali itayachukua na kuviweka chini ya vyama vya ushirika kwa usimamizi wa serikali.
“Lengo letu ni kuliendeleza zao la chai, tutaenda kutafuta masoko ili Tanzania itajirike kupitia chai. Chai ni zao letu la siku nyingi hatuwezi kuliacha mtu mwingine atuharibie,” amesema.
Pia, amewahakikishia wakulima kulipwa madai hayo na wafanyakazi wa viwanda vya chai kulipwa maslahi yao. Kuhusu zao la parachichi Samia aliahidi kujenga vituo 50 vya kuhifadhi parachichi kwa miezi mitatu ili kusubiri kupanda kwa bei ya soko, sambamba na vituo 50 vya kuhifadhia mbogamboga.
Pia, serikali itagawa bure miche 1,000 ya parachichi na kuajiri maofisa ugani mahususi kwa zao hilo Samia aliwahakikishia wakulima wa mikoa ya Songwe, Mbeya,
Njombe na Iringa kuwa serikali itafungua vituo vya kununua mahindi kupitia Wakala wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) ili kudhibiti ulanguzi.
Samia alisema mwelekeo wa serikali yake endapo itapewa ridhaa ya kuongoza nchi kuimarisha ushirika na vyama vya ushirika ili viweze kutafuta mitaji, vijitegemee na kujiendesha kibiashara kwani ndio njia ya kumfanya mkulima afaidi nguvu na jasho lake na ndio kumuinua mkulima.
“Pia, vyama vya ushirika vitatafuta mikopo, vitasambaza pembejeo kwa wanachama wake, watanunua mazao kwa wanachama wake, watatafuta masoko ndani na nje kwa mazao wanayolima lakini pia kujenga maghala ya kuhifadhia mazao yao, huko ndiko tunakotaka kuelekea,” amesema.
“Ni wahakikishie kwamba tumejipanga vyema kuvilea vyama vya ushirika na ushirika ndani ya nchi yetu, lengo ni kumfanya mkulima afaidi nguvu na jasho lake na huko ndiyo kumuinua mkulima.”
Amesema jambo ambalo watalisimamia ni kuhakikisha vyama vinaongozwa na watu mahiri na kuwa na matumizi ya mifumo ya kieletroniki katika kusimamia na kuendesha ushirika ili kuongeza uwazi hususani kwenye masuala ya mapato na matumizi.
Kuhusu shughuli za ufugaji, Samia kutokana na ufinyu wa ardhi na kuondoa migogoro kati ya wananchi na hifadhi ya Ruaha, Samia aliahidi kugawa Ranchi ya Usangu kwa wafugaji ili waendeshe shughuli zao.
Pia, ameahidi ujenzi wa machinjio ya mifugo ya kisasa inayojengwa Utengule na kuendelea na kampeni ya chanjo na utambuzi wa mifugo yenye lengo la kuongeza hadhi ya mifugo kutoka Tanzania katika masoko ya kimataifa.
Samia pia ameahidi kurejesha shamba la Mbarali Estate kutoka kwa mwekezaji na litagaiwa kwa wananchi na kusisitiza kuwa shamba hilo si kwa ajili ya viongozi bali ni la wananchi.
Pia, aliahidi serikali yake itaanzisha kongani za viwanda ambavyo vitasaidia vijana kupata ajira na kuongeza thamani ya mazao ya kilimo, mifugo, uvuvi, madini na misitu.
Kuhusu sekta ya miundombinu, Samia ameahidi kumaliza msongamano wa malori katika barabara inayounganisha Tanzania na Zambia (TANZAM) ambayo imechangiwa na ongezeko la mizigo katika Bandari ya Dar es Salaam kwa kuja na mikakati mitano.
Ameitaja mikakati hiyo ni kupanua kwa njia nne barabara hiyo ya urefu wa kilometa 75 kuanzia Igawa hadi Tunduma na kuifanyia ukarabati mkubwa Reli ya Tanzania na Zambia(TAZARA).
Pia, kukamilisha ujenzi wa bandari kavu yenye ukubwa wa ekari 1,800 katika eneo la Kasenjele mkoani Songwe, kuongeza barababara mbadala kuanzia eneo la Mwakabanga, kuongeza eneo la maegesho ya kisasa, kuongeza mizani ili malori yapime haraka na kuhakikisha nyaraka zinachakatwa kabla ya magari kufika mpakani.
“Pia serikali na mamlaka za Zambia tumeanza mazungumzo ili mamlaka za ukusanyaji mapato ya Zambia na wenyewe wafanye kazi saa 24 kama inavyofanya TRA ili huduma zitoke kwa haraka,” ameeleza.
Samia pia aliahidi kuwa serikali yake itahakikisha wilaya zote zinaunganishwa kwa barabara za lami na makao makuu ya mkoa. “Nimepokea maombi mengi katika mikoa yote ambayo nimepita, nikipata ridhaa ya kuunda serikali tutaendelea kujenga barabara za lami pamoja na changarawe ili zipitie muda wote,” amesema.
Ameongeza: “Kwa kawaida kila safari moja ya maendeleo huanzisha nyingine, ukijenga barabara moja ya lami watu wakionja raha ya lami wanadai na nyingine. Nataka niwaambie kwamba ujenzi wa kilometa moja ni sawa na Shilingi bilioni 1.2 ambayo ni sawa na vituo viwili vya afya, lakini hatutaacha kujenga.”
Aidha, kuhusu huduma za kijamii, Samia aliahidi kuimarisha huduma zinazogusa moja kwa moja wananchi ambazo ni maji, afya, elimu na umeme na kuwa utekelezaji wa huduma hizo hautakuwa na mjadala.
Kwa nishati ya umeme ameahidi kujenga njia ya kusafirisha umeme kutoka Iringa-Njombe hadi Tunduma ya kilovoti 730 na kati ya hizo kilovoti 400 zitatumika mikoa ya Njombe, Songwe na Rukwa huku kilovoti 330 zitauzwa Zambia.
Amesema pamoja na kusambaza umeme Tanzania nzima mijini, vijijini sasa nusu ya vitongoji vimefikiwa na nguvu inaelekezwa katika kuongeza uzalishaji umeme.
Uzalishaji umeme umeongezeka kutoka megawati 1,600 mwaka 2020 hadi megawati 4,000 mwaka huu na miaka mitano ijayo yamelenga kufikisha megawati 8,000 kwa kutumia vyanzo mbalimbali ikiwemo upepo na jotoardhi.
Eneo la afya, Samia alisema CCM ikipata ridhaa ya kuongoza nchi, itajumuisha huduma ya afya ya uzazi katika kitita cha huduma muhimu na itawahudumia wasio na uwezo.
Alisema pia serikali itatenga fedha na kuziweka kwenye mfuko maalumu wa kugharamia matibabu na vipimo maalumu vya kibigwa kwa wananchi wasio na uwezo.
Samia alisema watakamilisha miradi yote ya maji ili wananchi wapate maji safi na salama na wanawake wanakopesheka na wanatumia nishati safi kupikia.
Aidha, Samia hakuwasahau wafanyabiashara wadogo maarufu wamachinga na kuahidi kujenga soko la kisasa la Machinga Complex ndani ya mji wa Iringa.
“Niwahakikishie kuhusu dhamira yetu kuwaboreshea mazingira ya kufanya biashara zenu, nitakwenda kufanya hivyo,” amesema.



