Samia aacha ahadi 8 kisiwani Unguja
MGOMBEA urais Kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan leo anatarajiwa kuomba kura kwa wananchi kisiwani Pemba.
Samia tayari ameacha ahadi nane katika Kisiwa cha Unguja.
Akiwa Unguja amefanya mikutano miwili ukiwemo uliofanyika Uwanja wa Kajengwa, Jimbo la Makunduchi, Wilaya ya Kusini mkoani Kusini Unguja na uliofanyika Uwanja wa Hamburu, Jimbo la Nungwi, Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Samia amesema mgombea urais wa Zanzibar kupitia CCM, Dk Hussein Mwinyi ni mgombea sahihi atakayeshirikiana naye kuleta maendeleo kwa manufaa ya pande mbili za Muungano.
SOMA: Samia: CCM tutakuza kipato binafsi
Amesema pamoja na sera za fedha na uchumi kuchangia ukuaji wa uchumi wa asilimia 7 kwa Zanzibar na asilimia 6 kwa Tanzania Bara atakuza uchumi huo hadi kufikia zaidi ya asilimia 7 ndani ya mwaka mmoja kwa upande wa Tanzania Bara.
Samia amesema utulivu wa kisiasa ni muhimu kwa maendeleo ya nchi hivyo ameahidi kuendelea kuimarisha ulinzi na usalama wa nchi huku akiwasisitizia Watanzania kuwa uchaguzi si vita.
“Tunaingia kipindi cha uchaguzi, ninawaomba sana, twende tukadumishe amani, uchaguzi siyo vita, uchaguzi
ni tendo la kidemokrasia na watu kwenda kwa utaratibu tuliokubaliana,” amesema.
Ameongeza: “Sasa si muda wote kushika silaha kunaleta suluhisho. Muda wowote kushika silaha iwe ya moto au ya kimila hakuwezi kuleta suluhisho. Niwaombe sana amani na utulivu wa nchi ni jambo la muhimu zaidi kuliko mengine”.
Aidha, Samia amewatoa hofu Watanzania akisema: “Niwatoe hofu ndugu zangu wa Zanzibar na Watanzania kwa ujumla kwamba vyombo vya ulinzi na usalama vimejipanga kulinda nchi yetu. Sasa hutaki kishindo, kapige kura rudi nyumbani tulia, tumejipanga vema.”
Aidha, Samia pia ameahidi kuendelea kudumisha tunu za Muungano ambazo ni umoja, amani, utulivu na
mshikamano ambazo ndizo zimejenga taifa na utambulisho wa kipekee kimataifa.
Hivyo aliahidi kuanzisha kituo cha kumbukumbu na nyaraka za Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ili kiwe kituo ambacho vijana watajifunza masuala ya Muungano.
Pia, Samia ameahidi kuweka mazingira yatakayochangia kila Mtanzania hususani vijana wawe na shughuli ya
kuwaingizia kipato lengo likiwa ni kukuza kipato cha mwananchi mmojammoja.
“Katika kujenga Taifa linalojitegemea, hatutafika huko mpaka kila mtu ndani ya Tanzania yetu, kila kijana awe na shughuli inayompa kipato, yeye mwenyewe asimame kama mtu mmoja, ajitegemee halafu kwa ujumla wetu tunaweza kujitegemea,” amesema.
Ameongeza: “Na hii ndiyo kazi tunayoiendea, tunatakachokifanya ni kuandaa mazingira kwa vijana wetu kwa Watazania kuweza kuwa na shughuli za kufanya, kuingiza kipato ili kila mmoja ainue ustawi wa maisha yake.”
Pia, ameahidi kuendeleza juhudi za ukuaji wa sekta ya utalii sambamba na kuaza utekelezaji wa awamu nyingine ya programu ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) ili kuendelea kunyanyua maendeleo ya watu.
Pia, ameahidi kuendeleana utekelezaji wa miradi kupambana na mabadiliko ya tabianchi sambamba na eneo lingine la kipaumbele la uchumi wa buluu hususani uvuvi katika bahari kuu, kuimarisha usafiri na usaririshaji majini na suala la mafuta na gesi ili kunufaisha pande mbili za Muungano.
Samia apia ameahidi kurasimisha biashara ndogondogo kwa Tanzania Bara na Zanzibar na kuendelea kuwezesha kimitaji vikundi vya wajasiliamali.
Amesema pia serikali hizo mbili zitaendelea kukuza uhusiano wa kidiplomasia ili kuendelea kukuza jina la Tanzania ulimwenguni.
Mkutano wa kampeni umepangwa kufanyika katika Viwanja vya Gombani ya Kale ambapo wana CCM na wananchi watapata fursa ya kusikiliza ahadi za mgombea huyo.
Aidha, bendera za CCM na mabango yenye picha ya Samia yamepambwa na kupendezesha mitaa mbalimbali ya Kisiwa cha Pemba.
Juma Amer Juma, mkazi wa Chakechake amesema ana shauku ya kusikia ahadi zitakazotolewa na mgombea wa CCM hasa zile ambazo zitafungua uchumi wa kisiwa hicho.
“Miradi mingi ya maendeleo imetekelezwa katika mikoa hii yetu miwili, ni imani yangu hata kesho (leo) mengi atatuahidi ambayo yatazidi kuchochea uchumi wetu, na sina shaka na kwa atakachokiahidi anakwenda kukitekeleza.”
Aziza Omary Jumaa amempongeza Samia kwa kuendelea kuimarisha ulinzi na usalama katika kisiwa hicho.



