Samia aacha tabasamu mikoa ya Kaskazini

MGOMBEA urais wa Tanzania kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan amemaliza kampeni katika mikoa ya Kaskazini.

Katika mikutano ya kampeni kwenye mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara, Samia ametoa ahadi kadhaa kwa lengo la kukuza uchumi na kuboresha maisha ya wananchi.

Amesema wananchi wakimchagua serikali yake itafufua viwanda nchi nzima na vitaendeshwa na vyama vya ushirika na wawekezaji wengine.

“Mtakumbuka miaka ya nyuma mji wa Moshi ulikuwa na viwanda vingi vya kimkakati ambavyo baada ya ubinafsishaji viwanda vingi vilishindwa kuendelea na uzalishaji na kuwakosesha vijana wetu ajira, na hii ni changamoto ya maeneo mengi ndani ya nchi yetu,” alisema Samia.

Wakati wa mkutano wa kampeni kwenye Viwanja vya Mashujaa mjini Moshi, Samia alisema serikali imeviimarisha vyama vya ushirika kiasi hivyo vinaweza kusimamia, kushughulika na vyama vidogo vya ushirika na kuendesha viwanda.

Aidha, alisema serikali imefufua Kiwanda cha Kilimanjaro Machine Tools kilichokuwa kimesimama kwa zaidi ya miaka 30 na sasa kinatengeneza vifaa kwa ajili ya viwanda vingine.

Samia alisema miradi mingine ya kimkakati itakayochochea uchumi wa Moshi na nchi kwa ujumla ni ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kutoka Tanga hadi Musoma.

“Reli hii itapita hapa Moshi, itapita Arusha, mradi huu nao utakuja na fursa za ajira kwa wana Moshi na wana Arusha na utachochea zaidi biashara na uchumi katika ukanda huu wa kaskazini,” alisema.

Pia, Samia alisema serikali itakamilisha ujenzi wa barabara ya Holili-Tarakea yenye kilometa 53 ili kukuza biashara mpakani.

Akiwa Arusha aliahidi kukuza utalii kwa kuboresha usafiri wa anga, ujenzi wa kituo cha mikutano na mji wa michezo kwa ajili ya michuano ya fainali za Kombe la Mataifa Afrika (AFCON).

Alitaja mikakati hiyo kwenye mkutano wa kampeni katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha na akasema lengo la serikali ni kufikisha watalii milioni nane ifikapo mwaka 2030.

Samia alisema Kiwanja cha Ndege cha Arusha kimeboreshwa kwa gharama ya Sh bilioni 17 na kuanzia Januari mwakani kitatumika usiku na mchana.

Alisema wananchi wakimchagua serikali itaongeza ndege nane za Shirika la Ndege Tanzania (ATCL).

“Kingine ni utalii wa michezo, tumejenga uwanja kwa ajili ya mashindano ya Afcon lakini uwanja ule pia unakwenda kuwa kivutio cha watalii kwa sababu pale ulipo tutajenga kitu kinaitwa Mji wa Afcon, niwaambie kwamba uwanja ule tumeshaukamilisha kwa asilimia 63 na utakapokamilika utabeba watu 32,000 na mpaka Julai mwakani uwanja utakuwa umekamilika, tutaendelea na awamu ya pili ya ujenzi wa Kijiji cha Afcon,” alisema Samia.

Kuhusu kujenga kituo kipya cha mikutano cha kimataifa, Samia alisema wanakusudia kujenga kituo hicho kikiwa na hoteli na fursa zote za mikutano.

Pia, Samia alisema watajitahidi kuiweka vizuri miji ya Ngorongoro, Monduli na Karatu ili kuvutia watalii.

Alisema moja ya vipaumbele katika miaka mitano ijayo ni kuendeleza kongani za viwanda.

“Na kwa hilo katika mkoa wa Arusha tunakwenda kujenga kiwanda cha magadi soda kitakachokuwa Monduli na tayari mambo yanayohitajika yapo tayari tunasubiri kijengwe kwa hiyo ajira zitakwenda kuwa nyingi kwa vijana huko,” alisema.

Kuhusu kilimo, Samia ameahidi serikali yake ya CCM kuendelea kutoa ruzuku kwenye pembejeo za kilimo na kuufanya Mkoa wa Manyara uvune ngano tani milioni moja mpaka kufikia mwaka 2030.

“Nawaahidi kuwa tutaendelea kuleta pembejeo za ruzuku ili tuweze kuzalisha zaidi lengo letu kitaifa tuzalishe tani milioni moja itoke Hanang ili tuweze kujitegemea kwa mahitaji ya ngano, kilimo kikubwa huku ni ngano kwa hiyo tunataka Hanang ituzalishie ngano,” alisema alipofanya mkutano wake kwenye Uwanja wa Mount Hanang.

Mbali na kutoa ruzuku za pembejeo katika kufanikisha hilo, Samia alisema hatua nyingine watakazochukua ni kushughulikia mashamba ambayo wawekezaji wameshindwa kuyaendeleza.

Aidha, alisema Mkoa wa Manyara ni wanufaika wa ujenzi wa vihenge vya kuhifadhia mazao vya gharama ya Sh bilioni 18 na lengo la serikali ni kuhifadhi nafaka nyingi zaidi kwa ajili ya chakula ndani ya nchi na kufanya biashara ya nafaka, kwa sasa vihenge hivyo vinahifadhi tani 40,000.

Alisema serikali imejenga bwawa na skimu ya umwagiliaji Mbulu lililogharimu Sh milioni 8.5 na imekamilika ikiwanufaisha zaidi ya wana Mbulu 2,400 wanaolima zaidi ya hekta 90.

Samia pia aliahidi serikali yake kutoa kipaumbele kwa wachimbaji wadogo kwenye madini kutengeneza ajira za vijana.

Alisema sekta ya madini ni muhimu na moja ya nguzo kuu za kukuza uchumi, hivyo serikali yake imejipanga kuyapa thamani madini.

Samia alisema serikali yake itaongeza wigo wa ukusanyaji mapato ya kodi kuondokana na mikopo ya manyanyaso na kwamba itakopa mikopo huru itakayoheshimu uhuru wa nchi

“Wana Mwanga kila tulichokiweka kwenye ilani ya uchaguzi tunajua fedha yake ya utekelezaji inatoka wapi lakini nataka niwaambie lingine tumeongeza makusanyo ya ukusanyaji na tunaendelea kuongeza makusanyo ya mapato ndani ya nchi yetu kuepuka nyanyaso za mikopo na misaada,” alisema.

Aliongeza: “Kwa hiyo tunajua hakika fedha itatoka wapi, tutakopa ndio lakini mikopo ambayo itaheshimu uhuru wa nchi yetu, hiyo ndiyo tutakayokopa”.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button