Samia aagiza Watanzania walio Iran, Israel kurudi nchini

RAIS Samia Suluhu Hassan ameagiza Watanzania wanaoishi Iran na Israel warudishwe nchini.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dennis Londo amesema wizara hiyo inaendelea kutekeleza maelekezo hayo kwa kuratibu mchakato wa kuwarudisha nyumbani Watanzania hao.

Londo alisema hayo bungeni Dodoma jana wakati akichangia taarifa ya hali ya uchumi, Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa 2025/2026 na mapendekezo ya bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha 2025/2026.

“Bado dunia ipo kwenye sintofahamu kutokana na machafuko yanayoendelea sehemu mbalimbali, hivi sasa familia nyingi katika nchi yetu ambao wana ndugu, jamaa au marafiki katika nchi za Israel na Iran wapo kwenye sintofahamu, hawajui hatma ya Watanzania ambao wapo huko,” alisema.

Londo alisema Watanzania 168 walikuwa nchini Iran na 495 nchini Israel.

“Hadi sasa serikali imewezesha kuwarudisha Watanzania 147, kati yao 42 kutoka nchini Israel na 65 kutoka Iran kuondoka katika maeneo hayo hatari na kurejea nchini na maeneo mengine ya kiusalama,” alisema.

Aliongeza: “Juhudi hizi zinatekelezwa kwa uratibu wa wizara na balozi zetu Tel Aviv (Israel), Cairo (Misri), Ankara (Uturuki), Kuwait na Abu Dhabi (UAE). Ni mategemeo yetu kuhakikisha kuwa kila Mtanzania anarejea nchini salama”.

Alisema Tanzania inalaani migogoro inayoendelea na inasisitiza umuhimu wa kushughulikia changamoto kwa njia ya kidiplomasia kwa kuzingatia makubaliano mbalimbali katika umoja wa mataifa.

Londo alisema diplomasia ya Tanzania ipo vizuri sana, Tanzania ipo salama kimataifa na demokrasia ipo juu.

“Idadi ya maombi ya mikutano ya kimataifa, idadi ya mikutano ya kimataifa inayoendelea hapa nchini, ziara za viongozi wa kimataifa kuja hapa nchini, maombi ya ndugu zetu ambao wanaona Tanzania ni sehemu salama ya kufanya mazungumzo yao amani ni viashiria vinavyoonesha diplomasia yetu ipo juu,” alisema.

Londo alisema wizara hiyo inaendelea kutekeleza maelekezo ya Rais Samia kwa kuzungumza na Wizara ya Viwanda na Biashara na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) ili mikoa na halmashauri zinazopakana na nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wawezeshwe kutumia fursa katika soko la jumuiya hiyo.

Alisema Tanzania imewezesha kutekelezwa kwa mitangamano ya kikanda likiwemo soko la pamoja la EAC na utekelezaji wa programu za mtangamano ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na ushirikiano wa utatu yaani SADC, EAC na Soko la Pamoja la Mashariki na Kusini mwa Afrika (COMESA) na Eneo Huru la Biashara Africa (AfCFTA).

Londo alisema Tanzania imejiimarisha katika jumuiya ya kimataifa na imeongoza ajenda kubwa za kimkakati duniani ikiwemo ya kusimamia matumizi ya nishati safi hasa Afrika.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button