Samia aahidi ajira 5,000 siku 100 za kwanza

KOROGWE: Mgombea urais wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Samia Suluhu Hassan, ameahidi kuwa endapo atapewa ridhaa ya kuendelea kuiongoza nchi, ataanza kwa kuajiri watumishi 5,000 katika sekta ya afya ndani ya siku 100 za kwanza.

Watumishi hao watasambazwa katika vituo vya afya vinavyoendelea kujengwa nchi nzima.

Ahadi hiyo ameitoa leo, Septemba 30, 2025, wakati akihutubia maelfu ya wakazi wa Korogwe, mkoani Tanga, ikiwa ni sehemu ya kampeni zake kuelekea Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, mwaka huu.

Akizungumzia suala la huduma ya afya, Dk. Samia amesema pia serikali yake itaendelea kuboresha huduma za bima ya afya ili kuhakikisha matatizo kama ya kushikiliwa kwa maiti hospitalini yanakomeshwa.

“Bima ya afya itakwenda kutuondolea lile tatizo la kishikilia maiti, mtu anapotangulia mbele za haki, malipo hayajalipwa, madaktari wanaoendesha hospitali wanazuia maiti mpaka malipo yalipwe, hivyo suluhu yake ni bima ya afya, kila mmoja wetu akiwa na bima ya afya, malipo yakilipwa kwa bima hakitakuwa na haja ya kuzuia miili iliyotangulia mbele ya haki” amesema Dk. Samia.

Akizungumzia kuhusu huduma ya maji, Dk. Samia ameeleza kuwa serikali imepiga hatua kubwa katika kuhakikisha wananchi wanapata maji safi na salama, na kuongeza kuwa juhudi za kumtua mama ndoo kichwani zinaendelea.

“Tumeinua upatikanaji wa maji, tumefanikiwa kumtua mama ndoo kichwani lakini bado hatujamaliza kuwatua wamama wote kuwatua ndoo kichwani, lengo letu ni kila mtanzania awe na maji safi na salama karibu, kwahiyo hii kazi bado inaendelea” amesema Dk. Samia.

Dk. Samia aliwataka wananchi waendelee kuiamini CCM kwa kuwa imejipanga kuendeleza maendeleo yaliyokwisha kuanzishwa, hususan katika sekta muhimu kama afya na maji.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button