Samia aboresha upatikanaji dawa nchini, ununuzi 98%

SERIKALI ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, imeboresha upatikanaji wa dawa nchi nzima, kwani kwa kipindi cha miaka minne ununuzi wa dawa umefikia asilimia 98, kiwango ambacho hakijawahi kufikiwa tangu kuanzishwa kwa Bohari ya Dawa nchini (MSD).

Msemaji wa Serikali ambaye pia ni Katibu Mkuu, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa amesema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma.

Alisema ndani ya kipindi hicho, MSD imevunja rekodi kwani imeimarisha upatikanaji wa dawa, vifaatiba na vitendanishi kwenye vituo vya kutolea huduma za afya kutoka asilimia 39 mwaka 2021/22 hadi wastani wa asilimia 79 mwaka 2024/25.

Msigwa alisema ufanisi huo umetokana na MSD kuboresha mifumo ya usafirishaji ambayo imesaidia kusogeza huduma ya dawa karibu na wananchi lakini pia uwekezaji mkubwa uliofanywa na serikali katika sekta ya afya.

“Awali vituo vya huduma ya afya vilipeleka maombi MSD na havikupata dawa zote, lakini sasa vituo hivyo vina uwezo wa kupata dawa kwa wastani wa asilimia 79,” alisema.

Katika kuboresha huduma za uzalishaji, ununuzi na usambazaji, katika kipindi cha miaka minne, alisema serikali imeipatia MSD Sh bilioni 642.1 kati yake bilioni 196.3 mwaka 2024/25 kwa ajili ya kusogeza huduma ya dawa kwa wananchi.

Mkakati huo wa MSD, alisema umeenda sambamba na kujenga vituo 10 vyenye bohari, na tayari imeanza ujenzi bohari ya Mtwara na ya Dodoma kubwa kuliko zote nchini, na ujenzi upo hatua za mwisho.

“MSD inajenga maghala katika kanda hizo kwa lengo la kusogeza dawa, vitendanishi na vifaatiba katika maghala hayo yatakayojengwa pia katika mikoa ya Mwanza, Tabora, Kilimanjaro, Tanga, Kigoma, Mbeya na Lindi,” alisema.

Msigwa alisema, MSD imeimarisha upatikanaji wa dawa, vifaatiba na vitendanishi kwa kuanzisha vituo vya kusambaza dawa na kuboresha mifumo ya kusafirisha dawa hizo.

Mifumo ya usafirishaji dawa kutoka bohari kuu hadi kwenye vituo hivyo, alisema MSD imetumia Sh bilioni 184.2 sawa na asilimia 70 ya Sh bilioni 264.5 ambazo zilizotengwa kwa ajili ya kusafirisha na kulipia dawa hizo.

Pia, alisema MSD katika kusambaza dawa hizo imeongeza mapato yake kutoka Sh bilioni 315 mwaka 2021 hadi bilioni 640 mwaka 2025 sawa na ongezeko la asilimia 103.

“Kutokana na uwekezaji huo, upatikanaji wa dawa katika maeneo mengi kunafanyika kutekeleza agizo la Rais Samia alilotoa wakati anahutubia watanzania kupitia Bunge 12 mwaka 2021 kwa katika kipindi cha utawala wake ataboresha huduma ya afya nchini,” alisema.

Alisema ili kufikia azima hiyo MSD imekuwa ikiboresha huduma za afya dawa, vifaatiba na vitendanishi kwa kununua bidhaa kwa wazalishaji wa ndani ambapo mwaka 2024/25 imetumia Sh bilioni 98.72.

Msigwa alisema, vituo vya kutolea dawa kwa umma vimeongezeka tangu mwaka 1994 MSD ilipoanza kutoa
huduma ya kunununua na kusambaza dawa kwenye vituo.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button