Samia ahimiza kampeni zizingatie utu

DODOMA : MGOMBEA urais wa Tanzania kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan ametoa mwito kwa vyama vya siasa viendelee kufanya kampeni za kistaarabu zinazozingatia utu wa Mtanzania.
Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Itikadi, Uenezi na Mafunzi, Kenani Kihongosi alisema Samia ameagiza kila Mtanzania awe mlinzi wa amani ya nchi kwa kuwa ni tunu ya Watanzania. “Tangu kampeni zilipozinduliwa mgombea amekuwa akisisitiza utu wa Mtanzania, kulinda, kuthamini na kuheshimu watu, kampeni zisizo na matusi, kampeni zisizo na kejeli, kampeni zisizo na kebehi ni kampeni zenye staha, lakini kampeni ambazo zinaunganisha taifa” alisema Kihongosi.
Aliwaeleza waandishi wa habari Dodoma jana kuwa Samia amekuwa akihimiza amani, umoja, upendo na mshikamano jambo ambalo Watanzania wamekuwa wakilihitaji kwa asilimia 100. “Watanzania tuna wajibu wa kulinda umoja tulionao, tuna wajibu wa kulinda taifa letu, tuna wajibu wa kushirikiana na serikali katika kuhakikisha kila mmoja anakuwa mlinzi wa amani ndani ya taifa letu,” alisema Samia.
Aliongeza: “Lazima tudumishe upendo, kuheshimu vyombo vyetu vya ulinzi na usalama, kuhakikisha endapo tunahisi tunaona kuna matishio, tunaona kuna changamoto, tuziwasilishe kwenye vyombo vinavyohusika ili tulinde umoja tulionao”. Kihongosi alisema CCM inasisitiza hivyo kwa sababu inaamini binadamu wote ni sawa na kinaamini katika utu na kazi na kwamba palipo na amani kuna maendeleo.
“Hivyo kumchagua Dk Samia Suluhu Hassan moja ni kuchagua maendeleo, pili ni kuchagua amani, tatu ni kuchagua utu, nne ni kuchagua umoja, upendo na mshikamano wa taifa letu, na chama pekee ambacho kinaweza kusimamia misingi ya amani na utulivu, chama kinachohubiri umoja, chama kinachohubiri upendo, lakini chama ambacho kimeleta maendeleo ya kweli kwa wananchi ni Chama Cha Mapinduzi,” alisema.
Akizungumzia tathmini ya kampeni za mgombea wao, Kihongosi alisema mpaka sasa amefanya mikutano 77 katika mikoa 21 kwenye kanda za Kati, Magharibi, Pwani, Kusini, Nyanda za Juu Kusini, Pemba na Unguja (Zanzibar) na Kanda ya Kaskazini. “Zaidi ya watu milioni 14.62 wamejitokeza kwenye mikutano moja kwa moja, watu milioni 31.6, wamefuatilia kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii,” alisema.SOMA: Samia : Wachimbaji wadogo kuula
Kihongosi alisema mahudhurio yamekuwa makubwa kwenye mikutano ya Samia hali inayoonesha mgombea huyo anavyokubalika na wananchi. “Imani ya wananchi kwa Dk Samia Suluhu Hassan siyo bahati wala mkumbo, bali ni imechagizwa na uongozi wenye mafanikio makubwa katika miaka minne aliyoshika usukani wa urais,” alisema.
Kihongosi alitaja baadhi ya mafanikio ya Samia ni kukamilika kwa Mradi wa Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere (JNHPP) na Reli ya Kisasa (SGR). Alisema Samia kesho anatarajia kuanza ziara ya kampeni Kanda ya Ziwa na kuwataka wananchi wa huko kujitokeza kwa wingi kumsiliza akiinadi ilani yao.