Samia amsifu Ndugai umahiri, ukomavu

RAIS Samia Suluhu Hassan amesema Spika wa Bunge mstaafu, Job Ndugai alikuwa kiongozi mahiri.
Rais Samia alisema hayo wakati wa ibada ya kuaga mwili wa Ndugai katika viwanja vya Bunge jijini Dodoma jana.
Alisema vyombo hivyo vilimuamini kutokana na ukomavu wake katika siasa na aina ya uongozi wake ulioamini katika demokrasia ya Bunge.
“Marehemu Job Ndugai aliaminiwa Tanzania na hata kimataifa ambako alishika nafasi mbalimbali katika vyombo vya kibunge duniani kama ilivyoelezwa katika wasifu,” alisema Rais Samia.
Alisema Ndugai alifanya mabadiliko makubwa katika Bunge alipokuwa Spika wa Bunge ikiwa ni pamoja na kusimamia ujenzi wa jengo lenye kumbi tisa za mikutano.
“Ongezeko la kumbi za mikutano eneo la Bunge limepunguza sana gharama zilizokuwa zikitumika kukodi kumbi za mikutano wakati wa vikao vya kamati,” alisema Rais Samia.
Alisema pia Ndugai aliwezesha Bunge kuunda kamati nne zilizokuwa na jukumu la kuishauri serikali kuimarisha usimamizi na udhibiti wa maliasili za chini zikiwemo almasi, tanzanite, gesi asilia na mazao ya uvuvi wa bahari kuu.
“Mapendekezo ya kamati hizo yalichangia kuimarisha udhibiti wa rasilimali hizo na kuongeza mchango wake katika pato la taifa,” alisema Rais Samia.
Alisema Ndugai alipenda na kuthamini maendeleo ya vijana kupitia sekta ya elimu na alisaidia vijana kufikia ndoto zao kupitia elimu.
“Bila shaka miongoni mwa wanaoomboleza hapa leo wapo vijana ambao kama si jitihada binafsi za Ndugai wasingeweza kuhitimu masomo yao ya ngazi ya juu,” alisema Rais Samia.
Alisema Ndugai alipambana na kufanikisha ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Bunge iliyopo Kikombo mkoani Dodoma.
Rais Samia alisema kiongozi huyo ameacha alama ambayo haitosahaulika katika Wilaya ya Kongwa kwa kusimamia huduma za jamii kwa kuongeza idadi ya shule pamoja na vituo vya afya pamoja na huduma ya umeme katika kipindi cha uongozi wake akiwa Mbunge wa jimbo hilo.
“Kongwa ya leo si ya mwaka 2000 kumekuwa na maendeleo makubwa sana mwaka 2000 kulikuwa na shule za msingi 50 na sasa zipo 131 ndani ya Jimbo la Kongwa,” alisema.
Aliongeza: “Shule za sekondari zilikuwa tatu na sasa zipo 45 vituo vya afya vilikuwa vitatu na sasa vipo 10, zahanati zilikuwa 12 sasa zipo 56 na umeme ulikuwa vijiji 10 tu sasa vijiji vyote vimefikiwa na miundombinu ya umeme, maendeleo haya yamechangiwa kwa asilimia kubwa na msukumo wake na namna alivyoipambania Kongwa”.
Rais Samia alisema Ndugai alipata heshima ya kuwekewa alama ya Soko ambalo liliitwa kwa jina lake mkoani Dodoma ‘Soko Kuu la Job Ndugai’.
“Alitamani sana kuweka alama nyingine ya kutangaza mchango wa Wilaya ya Kongwa katika harakati za ukombozi wa nchi za Kusini mwa Afrika ili iwe sehemu ya utalii wa kihistoria,” alisema.
Rais Samia ameagiza mamlaka zinazohusika na kufanikisha Kongwa kuwa sehemu ya utalii wa kihistoria kupitia msaada wake katika katika harakati za ukombozi wa nchi za Kusini mwa Afrika.