Samia ataja mambo 3 ulinzi mazingira

RAIS Samia Suluhu Hassan ametoa mwito kwa Watanzania waendelee kujenga utamaduni wa kulinda na kuhifadhi mazingira kwa hiari. Taarifa ya Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais – Ikulu, Bakari Machumu kwa vyombo vya habari imeeleza pia Rais Samia amehimiza Watanzania watambue ulinzi wa mazingira ni msingi wa uhai, maendeleo na usalama wa taifa.
“Rais Samia anahimiza wananchi, taasisi na wadau wa mazingira kushiriki kuendeleza ajenda ya uhifadhi wa mazingira, ikiwemo kupanda angalau mti mmoja nyumbani, shuleni, kazini au kwenye maeneo ya jamii,” ilieleza taarifa ya Machumu.

Taarifa yake kwa vyombo vya habari ilieleza kuwa Januari 27, mwaka huu Rais Samia ataongoza upandaji miti katika maeneo ya Bungi Kilimo na Kizimkazi, Unguja ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha siku yake ya kuzaliwa. Rais Samia alizaliwa Januari 27, 1960 katika Kijiji cha Kizimkazi Mkoa wa Kusini Unguja, Zanzibar.
“Zoezi hili lenye Kaulimbiu: “Uzalendo ni Kutunza Mazingira, Shiriki Kupanda Miti” linaakisi dhamira ya Mheshimiwa Rais Dk Samia katika kuendeleza ajenda ya taifa ya uhifadhi na utunzaji wa mazingira ikiwemo upandaji miti, ulinzi wa vyanzo vya maji, kuimarisha uoto wa asili na kuchangia kwa vitendo juhudi za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi,” alieleza Machumu.
Machumu alieleza kazi hiyo ya kupanda miti ni ishara ya uwajibikaji wa pamoja na inatoa fursa kwa kila mmoja kwa nafasi yake na mahali alipo kushiriki kulinda na kuenzi mazingira kwa manufaa ya sasa na kizazi kijacho. SOMA: Watoto wajifunze umuhimu wa mazingira



