Samia ataka ubunifu zaidi biashara TRC

RAIS Samia Suluhu Hassan ametaka ubunifu zaidi katika kufanya biashara ya usafi rishaji kwa kuboresha vitengo vya biashara na mauzo kama kuweka watu wenye weledi na ubunifu kwenye masuala ya biashara.

Rais Samia ameyasema hayo kwenye hafla ya kupokea mabehewa mapya na yaliyokarabatiwa pamoja na uzinduzi wa Bandari Kavu ya Kwala iliyopo wilayani Kibaha mkoani Pwani.

Alisema uzinduzi huo ni mwanzo wa safari ya nchi kuwa kitovu cha biashara kwa Kanda ya Afrika Mashariki na Kati na kwamba maendeleo hayo yanaonesha sura mpya ya Tanzania.

“Uzinduzi wa safari za treni ya mizigo ya kisasa ni ushahidi kuwa Tanzania imeamua kwa dhati kuimarisha mfumo wa usafirishaji wa mizigo kuanzia kwenye barabara, usafiri wa anga, maji na reli,” alisema Rais Samia.

Aliongeza kuwa Reli ya Kisasa ya SGR kutoka Bandari ya Dar es Salaam hadi Dodoma ni sehemu ya mkakati wa kitaifa wa kupunguza gharama za usafirishaji, kupunguza uchakavu wa barabara na kulinda mazingira.

Alisema kwa kutumia reli hiyo mzigo unaweza kutoka bandarini na kufika Kwala ndani ya dakika 45 hadi saa moja na kufika Dodoma ndani ya saa nne hadi tano.

Alisisitiza kuwa hayo ni maboresho makubwa ya kupunguza muda unaotumiwa na magari ya mizigo ambao ni wastani wa saa 30 hadi 35 kwenda Kwala ikiwa ni pamoja na saa 24 za kukamilisha kuingia na kutoka bandarini.

“Mradi huu unatarajiwa kupunguza msongamano wa malori katikati ya Jiji la Dar es Salaam, kuongeza ufanisi wa bandari na kupunguza muda wa ushushaji na usafirishaji wa mizigo,”aliongeza Rais Samia.

Alifafanua kuwa ili kuimarisha usafiri na usafirishaji wa mizigo, serikali imewekeza Sh bilioni 330 kwa ajili ya ununuzi wa mabehewa ya mizigo 1,430.

Aliiagiza Wizara ya Uchukuzi pamoja na Shirika la Reli Tanzania (TRC) kuhakikisha mabehewa hayo yanatumika ipasavyo katika shughuli za kibiashara.

Aliongeza kuwa kupitia mfumo wa watoa huduma binafsi, ni vyema TRC ikashirikiana na Mamlaka ya Reli ya
Tanzania na Zambia (TAZARA) kama mtoa huduma binafsi ili kufikia mtandao mkubwa zaidi wa mizigo.

Alizitaka mamlaka zinazosimamia usafiri na usafirishaji wa mizigo kuendelea kuhamasisha wadau wa sekta ya usafirishaji wa ndani na nje ya nchi kuchangamkia fursa hiyo ya kutumia miundombinu hiyo ya usafirishaji kwa kununua vichwa vya treni na mabehewa yao wenyewe.

“Hii ni fursa ya biashara hivyo tutoe fursa kwa sekta binafsi wenye uwezo wa nje au ndani ya nchi kuja na mabehewa na vichwa vyao na tukubaliane namna ya kufanya kazi. Serikali kazi yake kulaza miundombinu na sekta binafsi kufanya biashara,”alisema.

Kadhalika, Rais Samia aliitaka TRC kuhakikisha kuwa wawekezaji wote walioonesha nia ya uwekezaji hawakwamishwi ili kuleta ajira kwa vijana wa Kitanzania.

“Katika siku za usoni tunataka kuona mteja wa bandari popote alipo anaweza kuagiza mzigo wake kokote duniani na aweze kuchukulia Kwala kwa kutumia CIF,” alisema Rais Samia.

Vilevile alisema katika mipango ya baadaye, serikali itaunganisha Kituo cha Bandari Kavu cha Kwala na Bandari ya Bagamoyo iliyopo kilometa 60 kutoka Kwala pamoja na Bandari ya Tanga iliyopo kilometa 256.

Alieleza kuwa Bandari ya Kwala ni ya Kipekee Afrika na kwamba Tanzania ni nchi ya kwanza kuwa na mradi huo Afrika Mashariki.

Alisema Kongani ya Viwanda ya Kwala itakuwa na uwezo wa kuchukua viwanda zaidi ya 200 na kutoa ajira za moja kwa moja zaidi ya 50,000 na zisizo za moja kwa moja 250,000.

Rais Samia aliishukuru Serikali ya DRC kwa kuipa Tanzania ardhi yenye ukubwa wa hekta 60 katika eneo la Kasumbalesa, Kasamboindo na Kasenga. Amezisihi nchi zote ziendeleze maeneo zilizopatiwa ili kurahisisha mifumo ya kufanya biashara kwa watu.

Kwa upande mwingine, Rais Samia alitoa maagizo mahususi kwa Wizara ya Uchukuzi na taasisi zake kuhamishia shughuli zake Kwala hadi kufika Jumatatu ya wiki ijayo.

Aidha, aliitaka wizara hiyo kuondoa msongamano wa malori yaendayo Dar es Salaam na badala yake yaishie Kwala huku akiitaka Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kuhakikisha inajenga Kituo cha Polisi Kwala kutokana na ukubwa wa mradi huo.

Vilevile, aliitaka Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kuendelea na upanuzi wa Bandari ya Kwala ili ichukue mzigo zaidi huku akiitaka TRC kuhakikisha kunakuwa na vitengo muhimu vya utoaji wa huduma kama za usafirishaji wa mifugo na bidhaa hatarishi.

Aliitaka TRC ikamilishe Chuo cha Reli pamoja na kuboresha Chuo cha Bandari pamoja na kuyaunganisha maeneo yote na mifumo ya usafirishaji huku akisisitiza kuwa sheria zote za uzalishaji zifuatwe.

Aliwataka wananchi wa Mkoa wa Pwani na Watanzania kwa ujumla kujiandaa kikamilifu na Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, mwaka huu.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button