Samia ataka ulinzi baharini, awagusa wavuvi

RAIS Samia Suluhu Hassan amesema bahari ni eneo muhimu kwa usalama wa nchi hivyo Taasisi ya Sayansi ya Bahari ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSMIMS) itambue na kuwa waangalifu wa chochote wanachokiona baharini wanapokuwa wanafanya tafi ti na kujifunza.

Pia, ameagiza taasisi hiyo kuanzisha mafunzo kwa vitendo ya muda mfupi kwa wananchi wanaozunguka taasisi hiyo wanaojihusisha na shughuli za bahari ili kuwaongezea tija. Rais Samia alieleza hayo wakati wa uzinduzi wa Majengo ya Taaluma na Utawala ya Taasisi ya Sayansi za Bahari ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM -IMS) iliyopo Buyu Kisiwani Unguja.

“Msisahau bahari yetu ni eneo muhimu sana kwa usalama wa nchi yetu, hivyo mbali mtakayofanya ndani ya maabara zenu ndani ya majengo haya msiache kuwa waangalifu na chochote kile mtakachokutana nacho ndani ya bahari,” alisema. Rais Samia alisema jamii inayozunguka taasisi hiyo lazima inufaike moja kwa moja na uwepo wa taasisi hiyo kupitia ajira, huduma, biashara na shughuli za kijamii.

Amesema Zanzibar inategemea uchumi wa buluu kukuza pato lake na kuongeza fursa za ajira, hivyo taasisi hiyo itasaidia kuchochea na kufikia uchumi jumuishi. “Nawahimiza taasisi kuanzisha na kuimarisha mafunzo mafupi ya vitendo hususani kwa wananchi wanaozunguka maeneo ya chuo wanaojihusisha na shughuli za baharini ili waweze kuongeza tija kwenye kipato, maendeleo endelevu na kuchangia katika uchumi,” alisema.

Amesema kupitia tafiti na maarifa yatakayopatikana katika taasisi hiyo yatasaidia katika maamuzi ya sera yanayolinda rasilimali za bahari na kuongeza tija na kipato cha wananchi. Sambamba na hilo, Rais Samia aliitaka taasisi hiyo kuimarisha ushirikiano na sekta binafsi, taasisi za serikali na watu binafsi ili tafiti zitakazofanyika hapo zilete matokeo chanya kwa wananchi.

Amesema IMS ni taasisi muhimu katika kufanya utafiti zinazochangia katika uvuvi endelevu, uhifadhi wa mazingira ya Bahari, mabadiliko ya tabia nchi, utalii wa bahari na uchumi wa buluu. Ujenzi wa majengo hayo ni utekelezaji wa mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) uliopo chini ya Benki ya Dunia ambapo UDSM imepokea Dola za Marekani milioni 49.5 katika miaka mitano.

Upande wa taasisi hiyo kati ya fedha hizo zimewezesha ujenzi wa madarasa 10, ofisi 41, maabara itakayobeba wanafunzi 114, chumba cha kompyuta cha kubeba wanafunzi 35, bweni la wasichana lenye uwezo wa kubeba wanafunzi 40 na ukumbi wa mikutano wenye uwezo wa kubeba watu 150.

Nae Mkuu wa UDSM, Rais mstaafu Jakaya Kikwete alisema ujenzi wa taasisi hiyo ni kielelezo cha dhamira ya serikali ya kuwekeza katika sayansi na tafiti katika elimu ya juu kama msingi wa maendeleo endelevu. SOMA: Samia aahidi kicheko kwa wavuvi

Amesema Rais Samia ameleta suluhisho kupitia maono yake ya kuimarisha elimu ya juu na utafiti kupitia ujenzi wa majengo ya taasisi hiyo, akiomba serikali kujenga hosteli ya wanafunzi wa kiume, kumalizia hosteli ya wasichana na taasisi hiyo kupatiwa boti ya kujifunzia na kufanya utafiti.

Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo, Profesa Wiliam Anangisye amesema kukamilika kwa majengo ya taaluma na utawala katika taasisi hiyo kutachangia kwa kiasi kikubwa kuongeza idadi ya wataalamu wa masuala ya uchumi wa buluu nchini.

Amesema taasisi hiyo italeta manufaa ikiwemo kuongeza idadi ya wanafunzi kutoka 172 hadi 472 ongezeko la wanafunzi 300 kwa mwaka, kutanua wigo wa vijana wa Kitanzania kupata maarifa, kuimarika kwa tafiti hususani katika uchumi wa buluu na kuimarika kwa ufundishaji na ujifunzaji kutokana na uwepo wa maabara za kisasa. Pia, taasisi hiyo itaongeza uwezo wa kufundisha tafiti na ubunifu kwani itaongeza programu sita zinazohusu ukanda wa bahari.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button