Samia ateua majaji wane, ampangia kituo balozi
RAIS Samia Suluhu Hassan amefanya uteuzi wa majaji wa Mahakama ya Rufani, wenyeviti wa bodi na kumpangia kituo cha kazi balozi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dk Moses Kusiluka, walioteuliwa majaji Mahakama ya Rufani ni Jaji Latifa Mansoor ambaye kabla ya uteuzi alikuwa Jaji Mfawidhi Kituo Jumuishi, Morogoro.
Mwingine ni Jaji George Masaju ambaye kabla ya uteuzi alikuwa Jaji wa Mahakama Kuu na Mshauri wa Rais, Sheria na Jaji Dk Deo Nangela ambaye kabla ya uteuzi huo alikuwa Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga.
Pia, amemteua Jaji Dk Ubena Agatho ambaye kabla ya uteuzi huo alikuwa Jaji wa Mahakama Kuu, Divisheni ya Biashara, Dar es Salaam.
Dk Kusiluka alisema Balozi Dk Stephen Simbachawene amepangiwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Brazil akichukua nafasi ya Balozi Profesa Adelardus Kilangi ambaye amepangiwa majukumu mengine.
Rais Samia pia amemteua Uledi Abbas Mussa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kipindi cha pili na Profesa Zacharia Mganilwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Uongozi wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) akichukua nafasi ya Profesa Wineaster Anderson aliyemaliza muda wake.
Kwa mujibu wa Dk Kusiluka, uapisho wa majaji hao utapangwa baadaye.



