Samia atoa uhakika mradi kuchakata gesi

LINDI : MGOMBEA urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan amesema Mradi wa Kuchakata na Kusindika Gesi Asilia (LNG) kuwa kimiminika, upo pale pale. Samia alisema hayo kwenye mkutano wa kampeni katika Uwanja wa Ilulu mjini Lindi.

Alisema mradi huo ni mkubwa wenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 40 (zaidi na Sh trilioni 100) na hivyo serikali ilitaka kuwa na uhakika wa manufaa kabla ya kuanza utekelezaji.

“Anayewekeza lazima awe na uhakika wa fedha yake anayoiwekea itamzalishia kiasi gani lakini na sisi tunaoletewa mradi lazima tuwe na uhakika kwenye mradi huu tutapata nini, kutokana na maliasili yetu inayokwenda kutumika” alisema Samia.

“Tumezungumza sana kwa miaka miwili, sasa tunakaribia kukubaliana, tuko hatua za mwisho za kukubaliana. Baada ya kukubaliana kabisa, tutasaini mkataba na wanaanza utekelezaji mradi.

Mradi upo lakini tusingeweza kuwa na mradi usiokuwa na manufaa kwa taifa, lazima tuzungumze, tuelewane mradi tujue tunapata nini, wanapata nini na tunaendaje. Kwa hivyo, mradi upo pale pale,” alisema.

Ajivunia kazi iliyofanyika Samia alisema katika maeneo yote aliyopita, kazi imefanyika katika miaka mitano iliyopita kwenye sekta za kijamii na uchumi. “Kwa kweli kazi imefanyika, ingawa hakuna awamu ya uongozi itakayosema imemaliza yote, lakini katika kipindi hiki cha miaka mitano, kazi kubwa imefanyika na kama mtatupa ridhaa ya kuendelea, yaliyoasalia tunakwenda kuyamaliza katika awamu ya pili,” alisema.

Samia alitoa mfano wa usambazaji wa umeme ndani ya nchi, kwamba vijiji vyote vimeunganishwa na nusu ya vitongoji vimefikiwa na nishati hiyo. “Tunapokwenda awamu ya pili ya Serikali ya Awamu ya Sita, tutakwenda kumaliza usambazaji wa umeme. Kinachobaki ni mwananchi kuuza mazao yako na kuhakikisha unaingia ndani ya nyumba, ndani ya duka au ndani ya taasisi yake,” alisema.

Kuhusu huduma ya maji safi na salama, Samia alisema kitaifa imefikia wastani wa kati ya asilimia 87 hadi 90 kwa mijini na vijijini. “Sasa awamu ya pili ya serikali ya awamu ya sita, tunakwenda kumaliza tatizo la maji. Tunataka kuhakikisha kila mtanzania yupo karibu na maji safi na salama na huko tunakwenda kulimaliza lakini lazima pia tutunze vyanzo vya maji,” alisema.

Kwa upande wa sekta ya elimu na afya, Samia alisema kwa kuwa idadi ya watu inaongezeka, mahitaji yatakuwepo kila siku. Serikali yake itahakikisha inaendelea kujenga shule, zahanati, vituo vya afya na kupeleka vifaa tiba na dawa.

Kuifungua Kusini Samia alisema kwa Mkoa wa Lindi mambo mengi yamefanyika na ahadi yake ni kwenda kuufungua Ukanda wote wa Kusini wa Lindi, Mtwara na Ruvuma. Alitoa mfano kwamba, kwenye masuala ya usafiri na usafirishaji serikali yake imejitahidi kwenye barabara, ingawa haijamaliza na kazi inaendelea.

Samia alisema kwenye usafiri wa anga, tayari ujenzi wa viwanja vya ndege Mtwara, Ruvuma na Lindi na kuahidi kuendelea kuanza ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Lindi na ujenzi wa uwanja mdogo Kusini mwa mkoa huo. Kwa upande wa usafiri wa majini, nao wanajitahidi kuuimarisha na kuwa wanafikiria kujenga Reli ya Kisasa (SGR) kutoka Mtwara mpaka Nyasa mkoani Ruvuma, hatua ambayo itarahisisha usafiri wa abiria na bidhaa za mazao.

Ahadi kwa changamoto Samia alisema miundombinu ya barabara na madaraja na changamoto ya Tanzania nzima na kuahidi kuwa hilo ni kipaumbele namba moja kwa serikali yake, ambacho kinafanyiwa kazi. SOMA: Ahadi za wengine ni maigizo tu

Alisema kwa Lindi, serikali yake itamaliza barabara ambazo zimeanza na kuzijenga zile ambazo ziko kwenye ilani na zitajengwa kwa kiwango cha lami na zingine kwa changarawe. Kuhusu wanyamapori wakali na waharibifu, alisema imekuwa kilio maeneo mengi, hivyo serikali imeanza kulifanyia kazi kwa kuongeza askari na kununua ndege nyuki za kufukuza wanyama.

Samia aliahidi kuendelea kujenga Vyuo vya Ufundi Stadi (VETA) kila wilaya na akasema Mkoa wa Lindi utafaidika na uwepo wa vyuo vikuu vitatu na pia utajengewa chuo cha nishati na umeme, ambacho kitafundisha vijana watakaotumika kwenye mradi wa NLG.

Alisema serikali imekuwa ikiongeza bajeti ya Wakala ya Vijijini na Mijini (TARURA) ili kuimarisha mindombinu ya barabara za wilaya, ili kurahisisha usafirishaji wa mazao ya wakulima.

Kuhusu uvuvi, alibainisha kuwa ujenzi wa Bandari ya Uvuvi Kilwa unaoendelea utakapokamilika utatoa ajira 30,000 na kufungua fursa za viwanda vya kuchakata samaki kutokana na uwepo wa umeme wa kutosha ndani ya Lindi.

Samia alisema serikali pia imetoa mikopo kwa wavuvi, zikiwemo boti tisa zenye thamani ya Sh milioni 712 na katika kuwawezesha wavuvi na utunzaji wa viumbe hai, ina mpango wa kujenga vizimba pamoja na kiwanda cha kusindika samaki.

Pia, aliahidi kuimarisha ushirika ambao utakuwa na uwezo wa kuendesha viwanda vya kuongeza thamani mazao ya wakulima na kuendelea kusisitiza mpango wa kuanzisha vituo vya zana na kukodisha zana za kilimo na kutoa ruzuku ya pembejeo.

Madini Samia alisema sekta ya madini imekua kwa kasi na leseni zimeongezeka kutoka 1,034 hadi 1,983 huku akiahidi kujenga soko lingine la madini, ili Mkoa wa Lindi uwe na masoko mawili.

Miradi ya Masoko Samia alisema serikali imeanzisha mfuko wa masoko unaosimamiwa na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI). Hivyo, halmashauri zinaweza kukopa zijenge masoko, kisha kurejesha mikopo hiyo.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button