Samia autaja 2024 kuwa wa kihistoria

Rais Dk Samia Suluhu Hassan.

RAIS Samia Suluhu Hassan amesema mwaka 2024 ulikuwa mwaka wa kihistoria kwa Tanzania kutokana na mafanikio yaliyopatikana kutokana na mambo kadhaa ikiwamo hamasa ya wananchi kujiletea maendeleo.

Rais Samia alisema hayo katika salamu zake za kuaga mwaka 2024 na kukaribisha Mwaka Mpya wa 2025, ambako alisema ni mwaka wa kihistoria kwa sababu taifa liliadhimisha miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Vilevile, alisema pamoja na kuadhimisha miaka 60 ya Muungano, kuliadhimishwa pia miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar, miaka 60 ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania, miaka 60 ya Jeshi la Polisi na miaka 60 ya Mbio za Mwenge wa Uhuru.

Advertisement

Alisema ni fahari kwa Watanzania kufanya maadhimisho hayo yote huku nchi ikiwa salama yenye amani na utulivu.

Alivipongeza vyombo vya ulinzi na usalama kwa kazi kubwa ya kulinda nchi huku akiwashukuru Watanzania kwa kuendelea kudumisha amani na umoja wa kitaifa.

Rais Samia alisifu Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kufanyika kwa amani na utulivu na kuongeza kuwa kwa mara ya kwanza wagombea ambao hawakuwa na washindani ilibidi wapate ridhaa ya wananchi, kwa kupigiwa kura ya ndiyo au hapana na kuondoa rasmi utaratibu wa kupita bila kupingwa.

Kuhusu uchumi, alisema kati ya Januari hadi Juni, 2024 uchumi ulikua kwa asilimia 5.4 ikilinganishwa na asilimia 4.8 katika kipindi kama hicho mwaka 2023, huku deni la taifa likiendelea kuwa himilivu na mfumuko wa bei ukibaki ndani ya lengo la asilimia tatu, hali iliyochangiwa na sera madhubuti za kifedha.

“Tulishuhudia ongezeko la uwekezaji kutoka ndani na nje ya nchi. Kupitia Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kati ya Januari hadi Novemba 2024, tumesajili miradi ya uwekezaji 865 yenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 7.7 inayotarajia kuzalisha ajira 205,000,” alieleza Rais Samia.

Vilevile, alisema Mamlaka ya Maeneo Maalumu ya Uzalishaji kwa Mauzo ya Nje (EPZA) imetoa vibali vya kuwekezwa nchini viwanda vipya vikubwa 15 vyenye thamani ya Dola za Marekani milioni 235, vinavyotarajia kuzalisha ajira karibu 6,000 na kuuza nje bidhaa zenye thamani ya Dola za Marekani milioni 94 kwa mwaka.

Kwa upande wa mapato, Rais Samia alisema Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imekusanya Sh trilioni 21.276 kati ya Januari na Oktoba, 2024 sawa na asilimia 99.3 ya lengo sawa na ongezeko la asilimia 17.5 ikilinganishwa na makusanyo katika kipindi kama hicho mwaka 2023.

Katika diplomasia, alisema mwaka uliopita Tanzania ilizidi kuimarika na kuleta manufaa makubwa katika nyanja za kimataifa na kupata heshima ya kushiriki Mkutano wa G20 ambao pamoja na maamuzi mengine yaliyofanyika, pia uliazimia kuunga mkono jitihada za upatikanaji wa nishati safi, na uliazimia kuimarisha uwekezaji kwenye kilimo ili kuondosha njaa na umaskini duniani.

Rais Samia alisema mafanikio mengine yanatokana na ziara alizozifanya katika nchi 16 duniani na kuwezesha kujenga uhusiano wa kidiplomasia na kiuchumi.

Alitolea mfano ziara ya Jamhuri ya Korea ilifanikisha kupatikana fedha zenye masharti nafuu Dola za Marekani bilioni 2.5 kutekeleza miradi katika sekta za maendeleo.

Alieleza kuwa kupitia fedha hizo, serikali itajenga Kituo cha Kisasa cha Mafunzo ya Reli, Chuo cha Mafunzo ya Anga na Urubani, ujenzi wa kituo cha kusambaza umeme Nyakanazi, na kituo cha uchenjuaji wa madini na maabara za kisasa za vito.

“Miradi mingine itakayoangaliwa ni mradi wa uendelezaji wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Ujenzi wa Kongani ya Viwanda Bagamoyo, na Ununuzi wa Mabehewa ya Abiria na Mizigo kwa ajili ya Kipande cha Reli kutoka Mwanza hadi Isaka, Ujenzi wa Bandari ya Wete na Ujenzi wa Bandari ya Uvuvi Bagamoyo,” alieleza

Aliongeza kuwa fedha hizo pia zitatumika kwenye ujenzi wa Barabara Zanzibar, ujenzi wa Ukumbi wa Mikutano Zanzibar na Ujenzi wa Studio ya Filamu ya Kisasa na Kituo cha burudani mbalimbali kwa ajili ya ajira za vijana.

Mbali na hilo, ziara hiyo pia ilifanikisha kusainiwa kwa Mkataba wa masharti nafuu wenye Dola za Marekani milioni 163.6 kugharamia mradi wa Ujenzi wa Hospitali ya Binguni na Kituo cha Mafunzo ya Afya, Zanzibar.

Ziara nyingine ni ya China ambayo iliimarisha uhusiano wa kidiplomasia, ilifungua milango ya soko la bidhaa mbalimbali ikiwemo mihogo mikavu, soya, mabondo ya samaki, mazao ya baharini, asali, mashudu ya alizeti na pilipili.

Rais Samia alisema kuimarika kwa uchumi kumewezesha kuendelea kufanya mabadiliko chanya katika mifumo ya elimu msingi na sekondari hadi vyuo vya ufundi.

Alisema serikali imeendelea kusogeza huduma bora za afya karibu zaidi na wananchi, kutandaza zaidi miundombinu ya umeme, kusambaza umeme vijijini.

Pia, kutekeleza dhamira ya kumtua mama ndoo kichwani kwa kusimamia utekelezaji wa miradi 1,300 ya maji nchi nzima ambapo kukamilika kwa miradi hio kutasaidia kutimiza lengo la asilimia 95 mijini na asilimia 85 vijijini.

Akizungumzia changamoto za mwaka 2024, alizitaja kuwa ni pamoja na athari za mvua za El Nino na Kimbunga Hidaya, uhaba wa fedha za kigeni hususani Dola ya Marekani, na ajali za barabarani.

Kuhusu ajali, alifafanua, “Takwimu za Jeshi la Polisi Tanzania zinaonesha kuwa kati ya Januari hadi Desemba mwaka huu, nchi yetu ilishuhudia jumla ya ajali 1,735. Na ajali 1,198 kati ya hizo zilisababisha vifo vya ndugu zetu 1,715”.

“Hii ni idadi kubwa sana. Ndugu zetu wengine 2,719 walijeruhiwa katika ajali za barabarani. Asilimia 97 ya ajali hizi zimetokana na makosa ya kibinadamu, kubwa kabisa ikiwa uzembe wa madereva, uendeshaji hatari na mwendo kasi ambayo kwa pamoja ni asilimia 73.7 ya ajali zote,” alieleza Rais Samia.

Aliitaka Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na Jeshi la Polisi Tanzania kuongeza mikakati ya kuzuia ajali zinazosababishwa na makosa ya uzembe.