Samia awapa neno mawaziri wapya

RAIS Samia Suluhu Hassan amemmwagia sifa Mbunge wa Peramiho, Jenista Mhagama aliyefariki dunia kuwa alikuwa kiongozi mwenye moyo wa kujali maslahi ya taifa na kuwataka wabunge na mawaziri wapya kufuata nyayo zake wakati wa kutekeleza majukumu yao.
Akizungumza katika mazishi ya kitaifa ya Jenista jana jijini Dodoma, Rais Samia aliwataka wabunge na mawaziri hususani wale wapya kufuata nyayo za Jenista.
Alisema mafaniko ya bunge na taifa yanatokana na mshikamano wa wabunge wote bila kujali tofauti za kisiasa.
“Pia, mijadala inabaki katika misingi ya kistaarabu na kuhakikisha inalinda heshima ya bunge kama chombo cha uwakilishi na wananchi,” alisema.
Rais Samia aliwataka pia kutimiza wajibu wao kwa uadilifu kama alivyokuwa Jenista.
Alisema katika maisha anayoyafahamu kwa Jenista alikuwa ni kiongozi jasiri na mlezi wa wengi ndani ya bunge, serikali na aliyejitoa kwa dhati kuwatumikia wananchi wa jimbo lake na taifa kwa ujumla
“Katika maisha yake ya utumishi alisimama imara kutetea haki, maendeleo na ustawi wa watu aliwaongoza, alikuwa nguzo ya matumaini kwa wanawake na vijana na mfano wa uongozi uliotawaliwa na nidhamu, uadilifu na hofu ya Mungu,” alisema.
Alisema Jenista alikuwa mwalimu kitaaluma na mwalimu katika uongozi kwani alitumia kipawa chake kulea na kusimamia mawaziri akiwa mnadhimu na katibu wa kamati ya wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
“Wabunge na mawaziri walimuheshimu na yeye alijiheshimisha,” alisema.
Rais Samia alisema katika nafasi zake hizo ametoa mchango mkubwa katika chama, bunge na baraza la mawaziri.
“Yeye ndiye mtu pekee katika historia ya nchi yetu aliyewahi kuvaa kofia mbili ya katibu wa kamati ya wabunge wa Chama Cha Mapinduzi na mnadhimu wa serikali bungeni, na kofia hizo zilimtosha na kumuenea sawa.
“Jenista alikuwa mtu asiye na mzaha lakini mcheshi, alikuwa mtii kwa mamlaka zake, chama chake na wananchi wake, zaidi alikuwa mnyenyekevu kwa Mungu wake, mambo yaliyomfanya akapendwa na kuheshimiwa na watu walio chini yake na viongozi wenzake,” alisema.
Rais Samia alisema Jenista alipata fursa ya kufanya kazi chini ya uongozi wake na kumpa jina la ‘kiraka’ kwani kila alipomweka aliziba vizuri.
Jenista chini ya uongozi wa Rais Samia aliwahi kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu, Bunge, Vijana, Ajira, Kazi na Watu wenye Ulemavu, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na Waziri wa Afya.
Alisema pia alikuwa kiongozi anayesimama imara kutetea maslahi ya nchi bila kuchoka na bila kujali changamoto.
“Kupitia sauti yake bungeni, vitendo vyake katika jamii na msimamo wake katika uongozi ameacha kumbukumbu njema, ameandika hadithi nzuri kwa ajili yake. Tunatambua kuwa safari yake ya uongozi haikuwa rahisi lakini alitembea kwa ujasiri hekima na heshima.
“Leo tunapomuaga kuelekea makao yake ya milele tunabaki na kumbukumbu za tabasamu lake, hekima yake na moyo wake wa kujali maslahi ya taifa na nisema tumepoteza mtu muhimu sana,” alisema.
Aidha, Rais Samia alitoa pole kwa familia na kusema, “poleni sana, taifa lipo pamoja nanyi katika kipindi kigumu, tunawaombea faraja, nguvu na amani kutoka kwa Mwenyezi Mungu.
“Kwa wana Ruvuma, wana Peramiho tunawapa pole kwa kupoteza tumaini lenu, Mwenyezi Mungu awape faraja. Kwa spika, wabunge wote na wana CCM wenzangu nisema tumeondokewa na tupeane pole”.
Aidha, Rais Samia alituma salamu kwa Jenista akisema, “kwa mdogo wangu Jenista Mhagama tunasema, umetimiza wajibu wako kwa uaminifu mkubwa, umepigana vita vilivyokupasa, uimara wa taifa letu ni pamoja na mchango wako mkubwa, Mwenyezi Mungu akupe safari ya heri safari njema na ailaze roho yake mahali pema peponi.
“Tunamshukuru Mungu kwa maisha yako na yote uliyoyafanya kwa familia, jamii na taifa kwa ujumla”.
Kwa upande wake Makamu wa Rais, Balozi Dk Emmanuel Nchimbi alisema Jenista alikuwa mnyenyekevu na aliyependa watu wake.
Alisema katika maisha yake ya kazi alitanguliza kuwatumikia wananchi wake na hata alipoteuliwa kuwa waziri alionesha mapenzi kwa wananchi na kuguswa na wanyonge.
“Ndiyo maana leo hii wanyonge wa Peramiho wana uchungu zaidi kuliko mtu yeyote, kwa sababu wanajua mpiganaji wao, mtetezi wao ameondoka, ametangulia mbele za haki. Ni ombi letu kwamba wapate mtumishi mwingine wa aina yake,” alisema.
Dk Nchimbi aliongeza: “Wakati tukitafakari kifo cha Jenista nikawaza sana, nikasema kama Mungu angeniambia niombe kitu kimoja tu, ningeomba kwamba wabunge wote wa CCM, wabunge wote wa nchi hii, madiwani wote wapende na kuwatumikia watu wao kwa kiwango cha Jenista Mhagama”.
Akitoa salamu za shukurani mtoto wa Jenista, Victor Mhagama alisema Jenista alikuwa ni mama kwao aliyeunganisha familia na aliyewafundisha kuishi wakimtumaini Mungu.
Alisema alikuwa ni kiongozi aliyewalea wengi lakini aliyehimiza kufanya kazi kwa bidii na mzalendo aliyeipenda nchi yake.
“Siku zote alitaka kazi yenye matokeo, alikuwa mchapakazi na ametulea kufanya kazi na kuwa viongozi, alikuwa akitusisitiza tuipende nchi yetu kwani hatuna nchi nyingine, alikuwa ni mzalendo wa kweli.

“Miradi mingine imeenda Peramiho, ya shule, barabara kwa kweli huyu mama hana deni na mimi kama mwana Peramiho naweza kusema mama huyu ametusitiri na Mungu airehemu roho yake… nisema huyu mama hakuwa mama yetu sana, bali alikuwa mama wa taifa lote, alitumika vilivyo na alitumikia wengi, nashukuru sana,” alisema.
Naye Spika wa Bunge, Mussa Azzan Zungu alisema taifa limempoteza kiongozi mwenye uwezo, aliyependa kazi na nchi yake na mnyenyekevu.
“Tumwombe Mungu ampe pumziko la milele mbinguni pamoja na wapendwa wetu waliotutangulia… tunamshukuru Rais (Samia) kwa kusimama nasi katika kipindi hiki cha majonzi na kwa kutoa ndege ya kusafirisha mwili wa marehemu kwenda Songea kwa mapumziko yake ya mwisho,” alisema.
Zungu pia alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa wanafamilia kupendana na kamwe wasisikilize maneno yanayoweza kuwagawanya.
“Hakuna jambo ambalo Mungu analipenda kama umoja, na mna bahati kwa kuwa na mama mwenye roho ya upendo,” alisema.
Awali Katibu wa Bunge, Leonard Baraka alisema Jenista alifariki Desemba 11, mwaka huu katika Hospitali ya Benjamini Mkapa kutokana na maradhi ya moyo.



