Samia azindua boti za bil 4/- za wavuvi Tanga

RAIS Samia Suluhu Hassan amezindua boti 35 zitakazotumiwa na wavuvi wa Mkoa wa Tanga zenye thamani ya Sh bilioni nne ambazo ni sehemu ya mradi wa boti 120 wa awamu ya pili wenye thamani ya Sh bilioni 11.5.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Dk Ashatu Kijaji amesema kati ya boti 35 za Mkoa wa Tanga, boti 10 zitabaki katika Wilaya ya Pangani na kwamba boti zingine zitaifikia mikoa husika kabla ya mwaka huu kuisha.
Akielezea kwa kina mradi huo kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika jana wilayani Pangani mkoani Tanga, Dk Kijaji alisema boti 120 za awamu ya pili zimegawanywa katika makundi matatu ambayo ni Kanda ya Pwani iliyopata boti 70, Kanda ya Ziwa Victoria boti 29 na Kanda ya Tanganyika na Nyasa boti 21.
Aidha, Dk Kijaji alisema mradi huo utawagusa wavuvi wapatao 1,872 na kwamba umesaidia kukomesha uvuvi haramu baada ya vijana 113 kujitokeza kwa Mkuu wa Mkoa wa Tanga na kuahidi kuachana na uvuvi haramu.
“Wamejitokeza vijana wa Kitanga 113 wakaenda kujikabidhi kwa mkuu wa mkoa kwamba sasa wanaachana na uvuvi haramu na wanaomba kupewa boti ili wafanye kazi hii kwa uhalali kabisa,” alisema Rais Samia.
Aliongeza kuwa vijana hao wanaenda kuwa walinzi wazuri wa rasilimalli za nchi hususani rasilimali za maji.
Akiwasilisha salamu za wavuvi nchini, Dk Kijaji alisema wavuvi wamemshukuru Rais Samia kwa kuyagusa maisha yao kitu ambacho hawajawahi kukipata katika kipindi cha miaka 63 ya Uhuru.
Dk Kijaji alieleza kuwa katika mradi wa boti awamu ya kwanza serikali ilitoa Sh bilioni 11.5, ambako boti 160 zilinunuliwa na kugawanywa katika kanda tano za Pwani, Victoria, Tanganyika, Nyasa na Ziwa Rukwa.
Alisema katika ukanda wa Pwani, Mkoa wa Tanga ulipata boti 14, Pwani boti 88, Dar es Salaam boti tano, Lindi boti 32, Mtwara boti 18 na Pwani boti 19.
Waziri wa Maji, Jumaa Aweso ambaye pia ni Mbunge wa Pangani, alisema wananchi wa Pangani hawana mtu wa kumtumainia zaidi ya Rais Samia kwa kuwakumbuka baada ya kukaa wapweke kwa miaka zaidi ya 60.
Alisema baada ya Rais kuona wananchi wanavyoathiriwa na maji ya bahari, alitoa Sh bilioni mbili ukajengwa ukuta umewafanya wananchi wa Pangani kutomsahau Rais Samia.
Alisema wananchi wazee kwa vijana wa Pangani wamefurahishwa kwa kiasi kikubwa kutokana na ujenzi wa mradi mkubwa wa Barabara ya Pangani hadi Bagamoyo ambayo ilianza kuimbwa tangu utawala wa awamu ya kwanza.
Very shortly this site will be famous amid all blogging visitors, due to it’s pleasant articles or reviews