Samia kuhitimisha kampeni kesho Mwanza

MGOMBEA urais wa Tanzania kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan anatarajia kufunga kampeni za Uchaguzi Mkuu za chama hicho kesho mkoani Mwanza. Katibu wa CCM Mkoa, Omary Mtuwa amesema kampeni hizo zitahitimishwa katika Uwanja wa CCM Kirumba wilayani Ilemela. “Tunawakaribisha wananchi wote, wanachama wetu na wasiokuwa wanachama wa Chama Cha Mapinduzi,” alisema Mtuwa.

Amewaambia waandishi wa habari CCM imechagua kufungia kampeni mkoani humo kutokana na wingi wa wapigakura Kanda ya Ziwa na akabainisha ni takribani asilimia 38 ya wapigakura wote nchini na Mwanza pekee ikikadiriwa kuwa na wapigakura takribani milioni mbili. Mtuwa alisema kampeni za CCM zimefanyika salama wamewafikia wananchi wengi kama ilivyokusudiwa.

Kwa mujibu wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kesho ni siku ya mwisho kufanya kampeni kwa vyama vya siasa kabla ya kufanyika uchaguzi keshokutwa. Kwa mujibu wa taarifa ya CCM, mkutano wa kufunga kampeni unatarajiwa kufanyika kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

Mgombea urais kupitia chama hicho, Samia amezunguka mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar akiinadi Ilani ya CCM na kuomba kura. Samia amewahakikishia usalama wananchi waliojiandikisha kupiga kura keshokutwa. SOMA: Mwinyi ataja sekta 11 kipaumbele awamu ijayo

“Nendeni mkapige kura bila hofu kwani usalama ni wa kutosha, mambo mengine niachieni mimi… tokeni mwende mkapige kura… ninayeongea hapa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa nchi hii,” alisema kwenye moja ya mikutano yake mkoani Dar es Salaam.

Aliongeza: “Hakuna tishio la kiusalama litakalokuwepo, anayesema ni Amiri Jeshi Mkuu wa nchi hii, niwaombe ndugu zangu twendeni tukapige kura, baba ukitoka hakikisha unatoka na familia umekwenda kupiga kura, kila aliyeandikishwa.

Mabalozi wetu wa maeneo hakikisheni mmetoka na watu wenu wote kwenda kupiga kura… wote mliojiandikisha nendeni mkapige kura bila hofu yoyote. Mama (yeye) yuko macho anawalinda, vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vipo macho vinawalinda, kama yamewashinda wao sisi tupo tunaendelea na ujenzi wa nchi yetu”.

Samia alitoa wito kwa vijana wasikubalI kudanganywa wakaiharibu nchi yao. “Sisi wazazi wenu tunapita, nchi hii inawategemea nyinyi tunatarajia nyinyi (vijana) tuwaachie nchi hii muiendeshe kama tunavyoiendesha. Kwa hiyo vijana wa Tanzania msidanganywe hata kidogo na katika kuendesha nchi tumetengeneza mifumo mizuri ambayo kila baada ya miaka mitano tunachaguana namna ya kuongoza nani ashike nafasi gani, katika ngazi tofauti hakuna maeneo mengine wanangu,” alisema.

Aliongeza: “Nawaomba vijana wangu msiharibu nchi yenu, msiharibu amani ya nchi yenu fuateni serikali yenu inavyowaelekeza, fuateni katiba yenu inavyowaelekeza, fuateni sheria za nchi zinavyowaambia, zinavyotaka mtaishi kwa usalama, mtaishi kwa amani hamtasumbuliwa”.

Samia alisema anapohakikisha watu wanapata maji safi, watoto wanapata elimu mpaka uwezo wao, afya iko karibu na kila mtu, umeme upo na usalama wa nchi upo na kila kitu kipo, kazi iliyobaki ni kuuheshimisha utu wa Mtanzania. “Kwa hiyo sina uchungu ndugu zangu, sina uchungu wa kubeba matusi yote yanayotolewa kwa sababu nafanya kazi hii, sina uchungu hata kidogo wala sijutii,” alisema.

Aidha, katika kampeni hizo Samia alisema serikali ya chama chake inafuata yale aliyosema mwasisi wa nchi ambaye ni Rais wa Kwanza, Mwalimu Julius Nyerere aliyesema ili nchi ipate maendeleo inatakiwa kuwa na watu, ardhi, siasa safi na uongozi bora. “Sasa Chama Cha Mapinduzi tumeamua tujikite sana kwenye watu, tuendeleze watu, tuendeleze utu wa mtu, tuujenge utu wa Mtanzania tuuheshimishe utu wa Mtanzania.

Alisema katika makazi, Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) linaendelea kujenga makazi sehemu mbalimbali ili wananchi wapate makazi. Tayari kuna miradi iliyokamilika na ambayo inaendeela kujengwa kama Kawe, Morocco, Magomeni, Kigamboni, Mtoni kwa Dar es Salaam huku kukiwa na mradi wa nyumba 1,000 Dodoma.

“Kuhusu kukuza uchumi, serikali imefanya kazi nzuri sana, tumejenga uchumi mkubwa na uchumi mdogo… tunatoa mikopo watu wapate mitaji na fursa ya watu kufanya biashara zao, tumejenga masoko, stendi maeneo ya kufanyia biashara, mikopo ya asilimia 10 nako tumefanya vizuri,” alisema. Alitaja mambo mengine yaliyofanywa na serikali yake ni kutengeneza miundombinu ya barabara, anga, reli na majini.

“Mengine kwenye kujenga utu wa Mtanzania ni masuala ya haki ya mtu, haki ya Mtanzania… tumeimarisha vizuri muhimili wa tatu wa dola, sheria na mahakama sasa haki zinapatikana, mambo yapo vizuri, zamani kesi inaenda miaka miwili haijaisha, siku hizi mambo ni tofauti,” alisema.

Habari Zifananazo

One Comment

  1. Just started this 3 weeks ago, and I already received my first check of $3,677 — pretty cool! It’s not a get-rich-quick thing, but if you can use a computer and internet and give some time each day, you can totally do this too. I was honestly surprised how real and simple it turned out to be.
    just check.…………> https://Www.Smartpay1.site

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button