Samia kuwapa raha wakulima, wafugaji
MGOMBEA wa kiti cha urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan ameahidi kugawa ranchi ya Usangu kwa wafugaji na Shamba la Mbarali Estate litagawiwa kwa wananchi.
Akizungumza na wananchi katika eneo la Ubaruku, wilayani Mbarali, Mkoa wa Mbeya, Samia amesema hatua hiyo inatokana na ufinyu wa ardhi katika wilaya hiyo unaoibua migogoro kati ya wananchi na Hifadhi ya Ruaha.
Pia, amesema serikali imelirejesha Shamba la Mbarali Estate kutoka kwa mwekezaji na litagawiwa kwa wananchi.
SOMA: Rais Samia: Madeni wakulima wa chai yatalipwa
“Ufinyu wa ardhi ulikuwa unaibua mgogoro kati ya wananchi, hifadhi na serikali imeamua kurejesha shamba la mwekezaji la Mbarali Estate na kuligawa kwa wananchi. Kwa sasa tuko katika hatua za mwisho kufanya tathimini na baadaye tutaligawa kwa wananchi,” amesema.
Akizungumzia fidia, Samia amesema: “Natambua kuna madai ya fidia kwa wananchi, hivyo niwahakikishie kuwa tutakamilisha tathmini na wote ambao hajalipwa fidia watalipwa fedha zao kikamilifu.”
Kuhusu vijiji vilivyo karibu na Hifadhi ya Ruaha, amesema ni vitano ambavyo vitaondolewa kutokana na umuhimu wa hifadhi hiyo kwa taifa.
“Hifadhi ya Ruaha ni muhimu kwa taifa letu na ndiyo chanzo cha maji yanayotumika kuzalisha umeme kwenye mabwawa yetu. Tukiachia wananchi wakae na kuharibu, basi mabwawa yote hayatakuwa na kazi ya kuzalisha umeme. Kazi yote tuliyoifanya ya kupeleka umeme kwenye vitongoji haitakuwepo kwa sababu mabwawa yatakuwa yamekauka, tutakuwa na umeme kidogo ndiyo maana vile vijiji vitano lazima viondoke,” amesema.
Akitoa ahadi kwa miaka mitano ijayo, amesema watakamilisha ujenzi wa barabara za mitaa kwa kiwango cha lami ikiwamo Barabara ya Kagomba, Ukaguzi na Utego mpaka viwandani na kuongeza mtandao wa barabara wa lami katika maeneo ya Igawa, Rujewa, Igurusi, Ubaruku hadi Kapunga.
Samia alisema serikali imetumia Sh bilioni tano kujenga hospitali ya wilaya huku vituo vya afya vinne na zahanati tisa zikiwa zimejengwa.
Pia, serikali imejenga shule za msingi mpya 35 na sekondari 14 pamoja na kuongeza walimu na madarasa kwenye shule zilizopo, huku Sh bilioni 10 zikitolewa kutekeleza miradi ya maji ambayo visima vifupi 30 na virefu 23 vilichimbwa na kujengwa.
Akiwahutubia wananchi katika Uwanja wa Sabasaba mkoani Njombe, Samia amesema kuhusu miradi ya chuma na makaa ya mawe ya Liganga na Mchuchuma, serikali ipo katika hatua za mwisho kuanza utekelezaji wake na mwekezaji mpya na baada ya uchaguzi mradi utaanza na utasaidia vijana kupata ajira.
Kuhusu chai, Samia amesema serikali imeshamwekea mazingira mazuri mwekezaji wa viwanda na mashamba yaliyoko Iringa na Njombe ambaye ni Kampuni ya DL Group ili kuweza kufufua viwanda na kulipa wakulima madai yao na stahiki za wafanyakazi.
Pia, amesema serikali itafunga mitambo mipya na ya kisasa ili kuzalisha chaitiba, kufufua kilimo cha chai na kuinua uchumi wa wananchi.
Katika hatua nyingine, Samia amewataka wagombea wote waliopita kwenye mchujo kuungana ili waingie kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba wakiwa wamoja na nguvu moja.



