Samia kuzindua Dira 2050 yenye upekee

DODOMA; RAIS Samia Suluhu Hassan leo Julai 17, 2025 anatarajiwa kuzindua rasmi Dira mpya ya Maendeleo ya Taifa ya Mwaka 2050, akiwa Rais wa pili kufanya hivyo mara baada ya Hayati Benjamin William Mkapa kuzindua Dira ya Taifa ya 2025 mnamo mwaka 2000.
Uzinduzi huo unafanyika katika ukumbi wa mikutano wa Jakaya Kikwete mkoani Dodoma.
Kulingana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Profesa Kitila Mkumbo, Dira 2050 imeweka rekodi pia ya kuwa dira yenye kuzingatia maoni mengi zaidi ya wananchi ambapo takribani wananchi milioni 1.17 walifikiwa mmoja mmoja, wengine zaidi ya 20,000 walifikiwa kupitia makongamano na mikutano ya wadau mbalimbali sambamba na waliotoa maoni yao kupitia tovuti maalumu ya Tume ya Taifa ya Mipango.
Kuzinduliwa kwa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 kulingana na Tume ya Taifa ya Mipango kunafuatia hatua muhimu ya Baraza la Mawaziri la serikali ya awamu ya sita kuidhinisha dira hiyo pamoja na kuridhiwa kwake kwa mara ya kwanza katika Historia na Bunge la Tanzania kama sehemu ya kutoa kinga katika kutekelezwa kwake na kutokuachwa kando na serikali zitakaoongoza Tanzania kwa miaka 25 Ijayo.
“Kwa mara ya pili nchi yetu inazindua Dira ya maendeleo ya Taifa ambayo haina mwelekeo wa kiitikadi ya Chama cha siasa na Rais Samia Suluhu Hassan anakuwa Rais wa Pili kuandika Dira ya Taifa, Rais wa kwanza alikuwa Hayati Rais Benjamini William Mkapa,” amesema Profesa Kitila.
Pamoja na mambo mengine, malengo ya Dira mpya ya Taifa ya mwaka 2050 kulingana na serikali ni kuchochea kasi ya ukuaji wa uchumi jumuishi unaopunguza umasikini, unaozalisha ajira na kuchochea mauzo ya nje ya bidhaa, kuongeza tija katika uzalishaji sambamba na uongezaji wa thamani kwenye mifugo, madini, misitu pamoja na kilimo.
Aidha, takwimu za maoni ya wananchi yaliyokusanywa kuhusu Dira Taifa ya Maendeleo 2050 zinaonesha kuwa idadi kubwa ya wananchi waliofikiwa na timu ya kuchukua maoni ni vijana wenye umri kati ya miaka 15-35 sawa na asilimia 81 ya watu wote waliotoa maoni kuhusu dira hiyo
Akizungumzia mafanikio ya utekelezaji wa Dira 2025, Profesa Kitila alieleza kuwa tathimini imeonesha kuwa asilimia 69 ya Watanzania wanaamini kuwa nchi iko katika muelekeo sahihi, huku asilimia 76 wakiamini kuwa miaka 25 mbele nchi itakuwa na ustawi mkubwa zaidi katika sekta mbalimbali.
Tume ya Taifa ya Mipango imeeleza kuwa zaidi ya wageni 5, 000 wakiwemo wadau wa maendeleo, wakuu wa taasisi za umma na binafsi pamoja na viongozi mbalimbali wa kitaifa na kimataifa watashuhudia tukio hilo la kihistoria linalokuja kila baada ya miaka 25 nchini, akitoa wito kwa wananchi wa Dodoma na mikoa ya jirani kujitokeza kwa wingi hii leo kushuhudia tukio hilo la kihistoria nchini.



