Samia kuzindua jengo makao makuu ya mahakama Dodoma

DODOMA: KWA MARA ya kwanza katika historia, Mahakama ya Tanzania inatarajia kuzindua Makao Makuu yake jijini Dodoma, hatua inayolenga kuimarisha mifumo ya utoaji haki nchini.

Rais Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuzindua miradi mitatu ya Mahakama, ikiwemo jengo jipya la Makao Makuu ya Mahakama jijini hapa.

Jengo hilo lenye ghorofa tisa na ukubwa wa mita za mraba 63,244 linatarajiwa kuwa kubwa zaidi barani Afrika kati ya majengo ya makao makuu ya mahakama na kushika nafasi ya sita kwa ukubwa duniani.

Kwa mujibu wa Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Profesa Elisante Ole Gabriel, jengo hilo limejengwa kwa asilimia 100 kwa fedha za walipakodi, likigharimu jumla ya Sh bilioni 129.7.

Jengo hilo linajumuisha matawi matatu ya mahakama, ambayo ni Mahakama ya Upeo (Supreme Court), Mahakama ya Rufani, na Mahakama Kuu, huku ofisi za utawala zikiwa katikati ya majengo hayo.

“Kwa mara ya kwanza tangu uhuru, Mahakama ya Tanzania sasa inapata Makao Makuu yake rasmi. Hapo awali, jengo la Mahakama jijini Dar es Salaam halikuwa rasmi kwa makao makuu,” alisema Profesa Gabriel.

Aliongeza kuwa jengo hilo limejengwa kudumu kwa zaidi ya miaka 100 na lina mifumo ya kisasa ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), ikiwemo huduma zinazotumia akili bandia, maroboti ya kuwaongoza wageni, pamoja na sehemu ya kutua helikopta.

“Makao Makuu haya yatakuwa na moja ya vyumba vya uangalizi wa hali ya juu zaidi duniani, likishika nafasi ya pili kwa teknolojia yake. Mfumo mzima wa mahakama nchini utaunganishwa na jengo hili, kuruhusu ufuatiliaji wa mwenendo wa mashauri kwa wakati halisi na kuongeza usalama,” alifafanua.

Mbali na jengo hilo, Rais Samia pia atazindua Makao Makuu ya Tume ya Utumishi wa Mahakama yenye ghorofa sita, ambalo limegharimu Sh bilioni 14.3, pamoja na makazi 48 ya kisasa ya majaji yenye thamani ya Sh bilioni 42.3.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button