Samia: Tayari nimeona moshi mweupe!

MOSHI:Mgombea urais wa Tanzania kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi( CCM), Dk Samia Suluhu Hassan amesema wananchi mkoani Kilimanjaro wameonesha kwa vitendo kuwakubali wagombea wa CCM na kinachosubiriwa kwa sasa ni tarehe ya kupiga kura ili kuwapa ushindi wa kishindo.
Akizungumza leo Oktoba Mosi, kwenye mkutano wa kampeni zake kuelekea uchaguzi mkuu katika viwanja vya Mashujaa, Moshi Mjini, Dk Samia ameeleza kuwa mapokezi makubwa aliyoyapata wilayani Moshi Mjini ni ishara kuwa wananchi wamewapa imani kubwa wagombea wa CCM.
“Jana nilianza kampeni zangu mkoani Kilimanjaro kwa kuzungumza na wananchi wa Same nao walifurika kwelikweli, nikaenda Mwanga nako walijitokeza kwa wingi sana na leo nimefika Moshi yenyewe nimejionea wingi wenu, niseme tu Moshi leo mmenipa raha,” amesema Dk Samia.
Ameongeza kuwa kabla hata ya kufika Oktoba 29, 2025 siku ya kupiga kura wananchi tayari wameonesha kuwa watawachagua wagombea wa CCM kutokana na vipaumbele vilivyowekwa katika ilani ya chama hicho.
Katika hatua nyingine Dk Samia amesema ikiwa chama hicho kitapewa ridhaa kwa mara nyingine Serikali yake itakamilisha miradi mbalimbali iliyokwishaanza na kuanzisha mingine ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa ilani wa CCM.