SBL, NCT watoa mafunzo kuwezesha vijana

Uwekezaji katika vijana wa Tanzania: Kampuni ya Bia ya Serengeti & Chuo cha Taifa cha Utalii kuunda Sekta ya Utalii endelevu Kwa vijana wengi wa Kitanzania, kufanikisha ndoto ya kujenga taaluma kwenye sekta ya ukarimu na utalii huonekana kuwa mbali na ngumu. Hata hivyo, sekta ya utalii na ukarimu imeendelea kuwa sekta yenye nguvu na inayokua kwa kasi zaidi nchini.

Serengeti Breweries Limited (SBL) kwa kushirikiana na Chuo cha Taifa cha Utalii (NCT) wamejitokeza kuziba pengo hili kupitia mpango wao wa Learning for Life. Hii ni programu inayotoa mafunzo ya vitendo, ikiwapa vijana nafasi ya kubadili shauku yao ya ukarimu kuwa ndoto halisi.

Mkurugenzi wa Masoko wa Kampuni ya Bia ya Serengeti Christopher Gitau akimkabidhi zawadi Mkuu wa Chuo cha utalii cha Taifa Dk. Florian Mtey wakati bwa uzinduzi wa program ya ‘Learning for Life’ jijini Arusha mwishoni mwa wiki hii ikilenga kuinua sekta ya utalii nchini kwa kuwapa mafunzo vijana zaidi ya 150 wenye ndoto ya kuwa kwenye sekta hiyo.

Baada ya uzinduzi uliokuwa wa mafanikio jijini Dar es Salaam mwaka jana, ambapo vijana zaidi ya 100 walihitimu mafunzo na kupata ajira katika kampuni kubwa za utalii, programu hii sasa imepanua wigo wake hadi Arusha – kitovu cha utalii nchini Tanzania. Awamu hii ya pili ni kubwa zaidi, ikiwajumuisha wanafunzi 150.

Mafunzo haya ni ya vitendo na ya kina, kuanzia darasani hadi nafasi za mafunzo kwa vitendo katika vituo vinavyoongoza vya ukarimu na utalii. Diageo Bar Academy nayo inatoa kwa ukarimu moduli za Mixology (uchanganyaji wa vinywaji), huduma kwa wateja na uendeshaji wa baa. Zaidi ya ujuzi wa kitaaluma, wanafunzi pia hujifunza mawasiliano, uongozi na mbinu za kujijengea taswira binafsi – zana zinazowaandaa ipasavyo kwa soko la ajira.

Mkuu wa NCT, Dk. Florian Mtey, alisema: Mafunzo haya yanazidi darasa, yanawapa wanafunzi uzoefu halisi wa maisha na kujiamini kukidhi matarajio ya waajiri.

Mkuu wa Chuo cha Utalii Taifa, Dk Florian Mtey akizungumza wakati wa uzinduzi wa awamu ya pili ya porogram ya “Learning for Life” kwa ushirikiano na Kampuni ya Bia ya Serengeti jijini Arusha. Program hii inalenga kuwanufaisha vijana zaidi ya 150 jijini hapo.

Mkurugenzi wa Biashara wa SBL,  Christopher Gitau, naye aliongeza kwa kusema waajiri waliowaajiri wanafunzi wa kundi la kwanza wameridhishwa sana na matokeo; hakuna malalamiko, bali ni simulizi za mafanikio pekee. Tunatarajia hali kama hiyo pia Arusha.

Programu hii pia inatoa kipaumbele kwa wanawake na vijana wasio na nafasi, kwa kuweka mkazo kwenye ujumuishi. Wengi wa wahitimu wa awamu ya kwanza wamepata ajira za kudumu katika hoteli, nyumba za wageni na makampuni ya utalii, huku wengine wakichagua kuanzisha biashara zao binafsi na kujiajiri.

Ikiungwa mkono na serikali kama mfano bora wa ushirikiano kati ya sekta binafsi na ya umma, Learning for Life si ushirikiano tu kati ya SBL na NCT bali pia ni kichocheo cha kiuchumi kinachofungua milango, kuunda nafasi za kazi na kuleta matumaini kwa mustakabali wa vijana wa Tanzania.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button