Sekta ya nyama na mwanga wa matumaini

SEKTA ya mifugo nchini inang’ara kwa matumaini mapya ya kiuchumi ikionesha ukuaji mkubwa unaochangia katika pato la taifa na kutoa fursa za kipekee za ajira na mapato kwa mamilioni ya Watanzania.

Takwimu zilizowasilishwa bungeni Jijini Dodoma Mei 23, 2025 na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Dk Ashatu Kijaji katika hotuba ya bajeti ya wizara yake kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 zinathibitisha ongezeko la idadi ya mifugo na uzalishaji wa nyama huku serikali ikiweka mikakati kabambe ya kunufaika zaidi na rasilimali hii muhimu.

Kivutio kikuu cha hotuba ya Dk Kijaji ni ongezeko la ajabu la thamani ya uzalishaji wa nyama ambao umepanda kwa kiasi kikubwa na kufikia Sh trilioni 10,378,706,595,000 kwa mwaka wa fedha 2024/2025. Hii ni ongezeko la asilimia 9.4 kutoka tani 963,856.55 zenye thamani ya Sh trilioni 9,476,474,305,000 mwaka 2023/2024.

Ongezeko hili la tija limechangiwa na juhudi thabiti za serikali kuhamasisha wafugaji kuvuna mifugo yao kwa tija, kuimarika kwa udhibiti wa magonjwa ya mifugo, uboreshaji wa mbari za mifugo na kukua kwa soko la nyama la ndani na nje ya nchi.

Kwa mapato hayo ni dhahiri kuwa, sekta ya mifugo nchini inaendelea kushuhudia ukuaji mkubwa kwani takwimu mpya zilizowasilishwa bungeni Mei 23, 2025 na Dk Ashatu Kijaji zinaonesha ongezeko kubwa la idadi ya mifugo na uzalishaji wa nyama.

Katika mwaka 2024/2025, nyama ya ng’ombe ilizalishwa tani 666,227.02, mbuzi tani 150,014.29, kondoo tani 31,647.60, kuku tani 147,449.98 na nyama ya nguruwe tani 58,775.14. Takwimu hizi zinaashiria si tu mafanikio ya wafugaji, bali pia mwelekeo chanya wa kiuchumi unaotoa matumaini mapya kwa taifa.

Sambamba na ukuaji wa uzalishaji wa nyama, idadi ya mifugo nchini imeongezeka kwa kasi na hivyo kuchangia ongezeko la thamani ya jumla ya mifugo yote nchini kutoka Sh trilioni 30,489,866,668,000 mwaka 2023/2024 hadi kufikia Sh trilioni 33,216,845,677,000 mwaka 2024/2025. Ongezeko hili la thamani linatokana na kuongezeka kwa idadi ya mifugo katika makundi yote.

Takwimu za idadi ya mifugo zinaonesha idadi ya ng’ombe imeongezeka kwa asilimia 3.4 kutoka ng’ombe 37,913,129 hadi 39,241,375, idadi ya mbuzi zimeongezeka kwa asilimia 3.6 kutoka mbuzi 27,586,547 hadi 28,595,597 huku idadi ya kondoo ikiongezeka kwa asilimia 3.2 kutoka kondoo 9,373,407 hadi 9,658,880.

Kuku nao wameongezeka kwa asilimia 5.0 kutoka kuku 103,080,708 hadi 108,221,085. Kwa upande wa kuku, wale wa asili wameongezeka kutoka 47,391,131 hadi 49,754,408 na kuku wa kisasa nao wameongezeka kutoka 55,689,577 hadi 58,466,677.

Aidha, alisema nguruwe wameongezeka kwa asilimia 5.1 kutoka 3,901,096 hadi 4,131,962. “Ongezeko hili la mifugo ni kiashiria tosha cha fursa kubwa iliyopo kwa Tanzania kuwa mzalishaji na msafirishaji mkuu wa nyama katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati,” anasema Dk Kijaji.

Dk Kijaji anasisitiza dhamira ya serikali kutumia kikamilifu rasilimali za mifugo kukuza uchumi na kuboresha maisha ya Watanzania. “Lengo letu si tu kukidhi mahitaji ya ulaji wa ndani yanayoendelea kuongezeka, bali pia kujipatia mapato makubwa kutokana na masoko ya kimataifa,” anafafanua bungeni.

Hotuba imeweka mkazo mkubwa katika uongezaji wa thamani wa mazao ya mifugo kabla ya kuuzwa. Dk Kijaji anaeleza kuwa mauzo ya nyama ghafi hayaleti faida kubwa kama yalivyo kwa nyama iliyochakatwa na kuongezwa thamani.

“Tunataka kuona viwanda vyetu vya nyama vikichakata nyama na kuzalisha bidhaa mbalimbali zitakazokidhi viwango vya kimataifa na kuvutia wanunuzi kutoka masoko ya kimataifa yenye fursa kubwa, hasa Mashariki ya Kati,” anasema.

Vyanzo vinabainisha kuwa, serikali imejipanga kuimarisha ranchi zake zilizopo na kuanzisha mpya zitakazotumika kama vituo vya kuzalisha mifugo bora, vituo vya kufundishia wafugaji na maeneo ya kuendeleza tafiti za mifugo. “Viwanda hivi vitawezesha Tanzania kuchakata nyama yake na kuisafirisha nje ikiwa na ubora wa hali
ya juu na kwa bei nzuri,” anasema.

Dk Kijaji anatoa mwito kwa sekta binafsi kuchangamkia fursa hizi za uwekezaji katika ranchi za kisasa na viwanda vya nyama akisisitiza kuwa serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi kustawisha sekta hiyo.

Pamoja na mafanikio hayo, hotuba ya Waziri Dk Kijaji haikukosa kutambua changamoto zilizopo, ikiwemo tija ndogo ya uzalishaji kwa kila mnyama, udhibiti wa magonjwa, uhaba wa miundombinu ya kisasa, na matumizi madogo ya teknolojia katika ufugaji na uchakataji.

Serikali kwa msingi huo, inaahidi kuendelea kushirikiana na wadau wote, ikiwemo sekta binafsi, taasisi za utafiti na wafugaji wenyewe ili kukabiliana na vikwazo hivyo na kufungua milango mipya ya fursa kwa ukuaji endelevu
wa sekta ya mifugo.

Kwa takwimu hizi zinazotia moyo sambamba na mikakati ya serikali, sekta ya nyama iko katika nafasi nzuri kuchangia katika pato la taifa, kuongeza ajira, na kuinua kipato cha wafugaji na wafanyabiashara huku ikihakikisha upatikanaji wa nyama salama na bora kwa Watanzania na walaji wa kimataifa.

Ushirikiano kati ya serikali na sekta binafsi utakuwa nguzo muhimu kufikia malengo haya na kuiweka Tanzania katika ramani ya kimataifa kama mzalishaji mkuu wa nyama.

“Tunataka kuona viwanda vyetu vya nyama vikichakata nyama na kuzalisha bidhaa mbalimbali zitakazokidhi viwango vya kimataifa na kuvutia wanunuzi kutoka masoko ya kimataifa yenye fursa kubwa hasa Mashariki ya Kati,” alifafanua.

Hii inamaanisha uwekezaji mkubwa unahitajika katika viwanda vya kisasa, mifumo ya udhibiti ubora na vibali vya kimataifa vya usafirishaji. Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa Mwaka 2025/2026 inatoa dira mpya na thabiti kwa tasnia ya nyama nchini.

Kwa kuweka mkazo katika uongezaji thamani, uwekezaji katika miundombinu na kushughulikia changamoto zilizopo, serikali inatoa fursa kubwa kwa wafugaji, wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla kunufaika na rasilimali hii muhimu.

Ushirikiano huu kati ya serikali na sekta binafsi utakuwa nguzo muhimu katika kufikia malengo haya na kuiweka Tanzania kwenye ramani ya kimataifa kama mzalishaji mkuu wa nyama.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button