Sera, mitaala mipya elimu sasa rasmi

KUELEKEA kuanza safari ya mageuzi katika sekta ya elimu, Rais Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuzindua Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014, Toleo la 2023 na mitaala ilivyoboreshwa inayotoa majibu ya hoja za wadau, ikiwamo lugha ya kufundishia na matumizi ya Akili Mnemba (AI).

Wakati wa kulihutubia Bunge, Rais Samia alitoa ahadi kwa Watanzania kuwa serikali anayoiongoza itafanyia mageuzi makubwa ya sera ya elimu na mitaala na kuielekeza Wizara ya Elimu, Sayansi na Tekinolojia kulisukuma jambo hilo.

Akizungumza jana jijini Dodoma, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda alisema uzinduzi huo utafanyika Januari 31, mwaka huu na kusisitiza kuwa mageuzi yaliyopo kwenye sera ni makubwa na yanatekelezwa kwa awamu.

Advertisement

“Mabadiliko katika sekta ya elimu yanagusa vizazi na vizazi, ukamilifu wa utekelezaji wake kuanzia elimu ya awali hadi kidato cha sita utachukua muda kwa sababu tumeanza utekelezaji wake hatua kwa hatua, elimu ya awali, darasa la kwanza, la tatu, kidato cha kwanza,” alieleza Profesa Mkenda.

Alisema hatua ya kuzinduliwa kwa sera na mitaala ni kubwa inayokwenda kubadilisha mwelekeo wa nchi katika suala la elimu.

“Bado kuna watu tunawasikia wanatoa mchango kuhusu maboresho ya elimu, kuna hoja mbalimbali ambazo zinazungumzwa na sisi tunazifuatilia, yapo majibu ya hoja zote katika sera na mitaala mipya,” alifafanua.

Profesa Mkenda alitolea mfano wa mambo ambayo yamekuwa ni mjadala mkubwa ambayo ni ya Somo la Kiingereza ambalo kwenye sera, suala la lugha lipo na kwenye mitaala ni ufundishaji wa lugha.

“Kuna wanaozungumzia suala la Artificial Intelligence (Akili Mnemba), hili ni suala kubwa na ukienda kwenye sera utaona masuala ya Tehama na ukija kwenye mitaala utaona utekelezaji wake unavyofanyika,” alieleza.

Alisema sera inayotarajiwa kuzinduliwa imeipa uzito masuala ya sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati na pia mitaala inaeleza namna inavyotekelezwa.

“Kuna masuala ya kumuandaa mwanafunzi, sio tu kwenye ubora wa elimu, lakini kuwa na ujuzi unaomuandaa kwenye dunia ya sasa na mabadiliko makubwa yanayotokea duniani, kwenye sera utaona masuala hayo yanavyoshughulikiwa na kwenye mitaala utaona jinsi yanavyotekelezwa,” alisema Profesa Mkenda.

Alisema katika uzinduzi huo, wadau na viongozi 3,000 wanatarajia kuhudhuria na kusisitiza utaenda sambamba na maonesho ya taasisi mbalimbali za elimu.

Akifafanua zaidi, alisema kazi ya kufanya mapitio ya sera na mitaala imechukua miaka mitatu na imeshirikisha wadau wakiwamo wataalamu wa elimu, walimu, wanafunzi na wananchi wa kawaida.

Alisema mchakato huo ulihusisha kujifunza kwenye nchi mbalimbali na walitembelea kwenda kuangalia wanachofanya kwenye elimu ili kupata mbinu za kuboresha elimu ya Tanzania.

“Kazi ya kupitia sera imekamilika na sasa tunayo sera ya elimu hapa nchini ambayo inaitwa Sera ya Elimu na Mafunzo ya 2014 Toleo la 2023, na tayari imeshaidhinishwa na Rais kupitia kikao cha Baraza la Mawaziri. Mitaala pia, imefanyiwa mapitio na kubadilishwa kuendana na sera ambayo tunayo,” alisema waziri huyo wa Elimu.

Alisema ili kuleta ufanisi wa utekelezaji wa sera hiyo, serikali imeanza kuwapiga msasa walimu nchi nzima na inatarajia kuajiri walimu 4,000 wa masomo ya biashara.

Naye Naibu Waziri, Omar Kipanga alisema jambo hilo ni kubwa na ni kiu ya Watanzania kuona mageuzi hayo katika mfumo wa elimu nchini.