Serikali: Bima ya Afya kwa wote itarahisisha huduma
DODOMA; SERIKALI imesema kuanza utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa wote utawezesha makundi mbalimbali ya wananchi wakiwemo watoto kupata huduma za afya kwa urahisi pasipokuwa na vikwazo.
Majibu hayo yametokana na swali la Mbunge wa Ulyankulu, Rehema Migilla aliyetaka kujua serikali ina mpango gani wa kusaidia watoto kupata matibabu baada ya kufuta Toto Afya Kadi, wakati ikisubiriwa Sheria ya Bima ya Afya kwa wote.
Naibu Waziri wa Afya, Dk Godwin Mollel akijibu swali hilo, amesema mfumo wa kulipia bima za watoto kupitia Toto Afya Kadi umebadilika na kwa sasa unafanyika kupitia utaratibu wa shule na vifurushi vya bima ya afya vya Najali, Wekeza na Timiza, ambapo wanajiunga kupitia wazazi wao.
“Kuanza utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa wote utawezesha makundi mbalimbali ya wananchi wakiwemo watoto kupata huduma za afya kwa urahisi pasipokuwa na vikwazo,” amesema.