MKUU wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha amesema serikali inatambua, inaheshimu na kuthamini kazi na mchango mkubwa unaotolewa na madhehebu ya dini likiwemo Kanisa Katoliki.
Amewataka waumini kuendelea kumuombea baraka Rais Samia Suluhu Hassan na serikali yake ili aendelee kuwatumikia na kuwaletea maendeleo wananchi wake wakiwemo wa Shinyanga.
RC Macha ameyasema haya leo Desemba 19, 2024 wakati wa Misa ya Utolewaji wa Daraja la Ushemasi kwa Deusdedith Nkandi ambapo pamoja na mambo mengine amempongeza kwa hatua hiyo na kumuahidi kuwa serikali inamtegemea sana.
“Serikali inatambua, inaheshimu na inathamini sana mchango wa madhehebu ya dini zote likiwemo Kanisa Katoliki, na kipekee kabisa nimpongeze Shemasi Nkandi na nimuahidi tu kuwa serikali tutafanya naye kazi wakati wote na ukumbuke tu kuwa kwa kuwa wewe bado ni kijana tunakutegemea sana kwenda kuwasaidia vijana wenzio waweze kuishi maisha mema ya kumpendeza Mungu na wafanye kazi pia kwa juhudi,” amesema RC Macha.
Ibada hii ya kumpandisha daraja Shemasi Nkandi imefanyika katika Kanisa Kuu la Mama mwenye huruma lililopo Ngokolo Manispaa ya Shinyanga imeongozwa na Askofu Mkuu mstaafu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo akiwa na mwenyeji wake Askofu wa Jimbo Katoliki Shinyanga Mhashamu Liberatus Sangu.