MTWARA: Waziri wa Madini Anthony Mavunde amesema serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan imedhamiria kuwasaidia wachimbaji wadogo kupata taarifa sahihi za maeneo yao ili kuwaondolea changamoto ya kuchimba kwa kubahatisha.
Mavunde amesema hayo leo Februari 23, 2024 katika Kijiji cha Utimbe,Kata ya Lupaso,Wilaya ya Masasi Mkoa wa Mtwara wakati wa uzinduzi wa zoezi la eneo la majaribio la utafiti wa kina wa miamba yenye viashiria vya madini linalofanywa na Kampuni ya Tukutech LTD kwa ushirikiano na Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini (GST).
Amesema, wachimbaji wengi wadogo wamepoteza mitaji na nguvu nyingi kwa kukosa taarifa sahihi katika maeneo wanayochimba.
“Kupitia Vision2030 tutalifikia eneo kubwa zaidi la nchi yetu kwa kufanya utafiti wa awali wa viashiria vya miamba yenye madini ili kuwaongoza kwa usahihi wachimbaji wa Tanzania,”amesema
Amesema, serikali imenunua mitambo 15 ya uchorongaji ambayo itawahudumia wachimbaji nchi nzima baada ya kuwa wamepata taarifa za awali za viashiria vya miamba madini.
Nae, Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Jiolojia na Utafiti Madini(GST) Dk Mussa Budeba amesema taasisi yake imejipanga vyema kutekeleza zoezi la utafiti wa kina wa madini kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kwa lengo la kufikia kufanya utafiti wa kina kwa asilimia 50 kwa eneo la Tanzania ifikapo mwaka 2030.
Akitoa maelekezo ya awali Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya TUKUTECH LTD Mhandisi Tukupala Mussa Mwalyolo amesema kampuni yake ipo tayari kushirikiana na serikali katika kutimiza lengo la utafiti wa kina wa madini nchini ili kuchochea ukuaji wa sekta ya madini na kwamba wapo tayari kufanya kazi na wachimbaji wadogo nchini ili kuwapatia taarifa sahihi za maeneo yao.