Serikali kupitia upya sheria, mikataba ya uwekezaji

DAR-ES-SALAAM : SERIKALI imeanza kupitia kwa kina mikataba ya uwekezaji baina ya nchi mbili (BITs) na sheria zinazohusiana, ikiwa ni hatua ya kimkakati kulinda taifa dhidi ya madhara ya kisheria na kiuchumi yanayoweza kujitokeza katika usuluhishi wa kimataifa.

Hatua hiyo inalenga kubaini maeneo yenye mapungufu katika mikataba hiyo ili yawekwe sawa kabla ya kutokea migogoro, ikiwa ni sehemu ya mpango unaoratibiwa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje na wizara nyingine husika.

Akizungumza katika kikao kilichoandaliwa na Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Uswisi na Tanzania, Mkurugenzi Msaidizi wa Usuluhishi wa Ndani wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, David Kakwaya, alisema mapitio hayo yanazingatia fursa na changamoto katika usuluhishi wa migogoro ya uwekezaji nchini.

“Tunapitia vifungu vyenye udhaifu na kuzungumza na nchi husika, lengo ni kuhakikisha pale panapotokea mgogoro, Tanzania haipati hasara isiyostahili,” alisema Kakwaya.

Aliongeza kuwa mchakato huo unahusisha pia ushiriki wa Tanzania katika juhudi za kimataifa kupitia Tume ya Umoja wa Mataifa ya Sheria ya Biashara ya Kimataifa (UNCITRAL), kwa lengo la kuboresha mifumo ya utatuzi wa migogoro ya uwekezaji kwa haki, ufanisi na uwazi.

Kwa upande wake, Mhadhiri wa Shule ya Sheria ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Jacktone Koyugi, alisema ni muhimu mikataba hiyo kupitiwa upya kwani masharti mengi ndani yake yamekuwa yakiwabeba zaidi wawekezaji na kuiacha nchi katika hatari ya kupoteza kesi.

“Kuna tofauti kubwa kati ya masharti ya mikataba ya uwekezaji na sheria za kitaifa, jambo linalopelekea nchi nyingi kushindwa kesi,” alisema Dk Koyugi.

Naye Mtaalamu wa Usuluhishi wa Kimataifa kutoka Uswisi, Bernd Ehle, alisisitiza umuhimu wa kuimarisha uwezo wa ndani kwa kuwajengea uwezo majaji, wanasheria na wafanyabiashara kuhusu masuala ya usuluhishi ili kuendesha mashauri kwa ufanisi zaidi.

Alisema usuluhishi ni nyenzo muhimu ya kutatua migogoro ya kibiashara kati ya nchi mbili, na Tanzania inapaswa kujiimarisha katika eneo hilo ili kulinda maslahi yake ya kiuchumi.

SOMA: Tanzania, Msumbiji kimkakati biashara, uwekezaji

 

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button