SERIKALI imeahidi kuwawezesha wajasiliamali vijana na wanawake kwa kuwapatia maarifa, masoko, fursa za kijamii na kiuchumi ili kupiga hatua katika kujenga uchumi wa familia na jamii.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Ridhiwani Kikwete ametoa ahadi hiyo leo Novemba 15, 2024 kwenye uzinduzi wa Jukwaa la soko la Bidhaa zinazozalishwa na wajasiliamali wazawa wasichana na vijana la Panda linaloratibiwa na Taasisi ya Her Initiatives.
“Serikali inaamini ukisaidia makundi haya muhimu basi utakua umesaidia Jamii nzima. Hivyo ni jukumu la Serikali kuwawezesha ili kuleta ustawi wa jamii zetu,” amesema Waziri Kikwete.
Ridhiwani amesema atashirikiana bega kwa bega na Taasisi ya Her initiatives katika kuhakikisha inatekeleza majukumu yake ya kuwainua wajasiriamali hao.
Taasisi hii inajulikana kutokana na juhudi kubwa wanazozifanya duniani kuwanyanyua vijana na wanawake, ambapo wameshinda zawadi za utambuzi maeneo mengi ikiwemo ile ya Global Citizen inayotolewa Marekani na ile inayotolewa na Mfalme wa Ubelgiji.