Serikali na jitihada za kuongeza thamani ya kahawa

KAHAWA ni kinywaji maarufu duniani na ni moja ya bidhaa muhimu katika soko la dunia ikishika nafasi ya nne baada ya mafuta, dhahabu na gesi asilia.
Uzalishaji wa kahawa nchini umechangia upatikanaji wa ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja kuanzia kwa wakulima, viwandani na hata kwenye biashara za kimataifa.
Mauzo ya kahawa ya Tanzania nje ya nchi yameongezeka kufika zaidi ya Dola za Marekani milioni 230 kutoka Dola za Marekani milioni 140, sambamba na kuongezeka uzalishaji wa kahawa kutoka tani milioni 34 hadi kufikia tani milioni 85 mwaka jana.
Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe anasema kuwa kahawa ni miongoni mwa mazao ya biashara ambayo kumekuwa na mikakati mingi katika kuhakikisha uzalishaji unaongezeka na kuwa na viwanda vya kuongeza thamani ili kupunguza
mauzo ya zao hilo nje ya nchi.
“Tumeweka malengo ya miaka 10 ijayo, ni kuhakikisha asilimia 50 ya kahawa inayozalishwa Afrika inaongezewa thamani ili kupunguza mauzo ya kahawa ghafi nje ya nchi,” anasema.

Bashe anasema kuwa suala la kuongeza thamani kahawa kwa kutumia miundombinu iliyopo ni ajenda ya kudumu.
“Licha ya kuongezeka kwa uzalishaji wa kahawa kutoka tani milioni 34 hadi kufikia tani milioni 85 bado kuna changamoto ya uuzaji kahawa ghafi kutokana na ukosefu wa viwanda hali ambayo imekuwa ikichangia kupungua kwa mapato,”anasema Waziri Bashe.
Anabainisha kuwa thamani ya biashara ya kahawa duniani ni dola bilioni 500 na Afrika ina uzalishaji wa asilimia 50 lakini inapata dola bilioni 2.5 tu ya mapato yote.
Pia, anasema pamoja na kuzalisha kiasi kikubwa na kupokea kiasi kidogo bado uagizaji wa kahawa iliyosindikwa kutoka nje ni mkubwa.
“Licha ya kuwa wazalishaji wakubwa wa kahawa, tunauza bilioni 2.5 lakini tunaagiza kahawa zaidi ya Sh bilioni sita,” anasema.
Anasema kuwa miongoni mwa mikakati ambayo nchi imeweka ili kuongeza uzalishaji wa kahawa ni pamoja na kusambaza miche milioni 20 ya kahawa bure kwa wakulima.
Anasema kuwa usambazaji wa miche ya kahawa utachangia kuongeza uzalishaji. Pia, anabainisha kuwa ajira za kahawa zinatengenezwa shambani ikiwemo kukaanga, kubangua, kusaga, kufungasha na kuuza lakini kwenye mnyororo wa thamani kuna hatua mbili tu nyingine zote zinapelekwa nje ya nchi.
Tanzania imekuwa ikizalisha kahawa aina ya Arabika na Robusta. Maeneo ya kilimo cha Arabika ni Kilimanjaro, Arusha, Tanga, Iringa, Mbeya, Kigoma, Manyara, Mwanza, Katavi, Mara, Njombe, Songwe, Rukwa, Geita na Ruvuma.
Pia, kahawa aina ya Robusta inalimwa katika mikoa ya Kagera na Morogoro. Ni katika jitihada hizo za kuongeza uzalishaji na thamani ya zao la kahawa, Tanzania inatarajia kuwa mwenyeji wa Mkutano wa Tatu wa Nchi Zinazozalisha Kahawa Afrika (G25 African Coffee Summit).
Akizungumzia mkutano huo Waziri Bashe anasema unatarajiwa kufanyika Februari 21 mwaka huu jijini Dar es Salaam na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais Samia Suluhu Hassan.
Anasema mkutano huo unaoandaliwa kwa kushirikiana na Shirika la Kahawa la Afrika (IACO) utahudhuriwa na Wakuu wa Nchi zinazolima Kahawa Barani Afrika, Mawaziri wa Kilimo, Sekta Binafsi na Viongozi wa Taasisi za Kahawa katika nchi zinazolima zao hilo Afrika. Wengine ni wakulima na wadau katika mnyororo wa thamani wa Kahawa.
Anasema mkutano huo utaongozwa na kaulimbiu ya Mkutano huo ni ‘Kufungua fursa za ajira kwa vijana kupitia
uboreshaji wa Sekta ya Kahawa Afrika.”
Bashe anasema mkutano huo utatoa mwongozo wa jinsi ya kushirikiana na Umoja wa Afrika (AU) na Mashirika yake, Benki za Maendeleo za Afrika na taasisi nyingine za fedha ili kuunda programu zinazochochea ujasiriamali na ajira kwa vijana kupitia Sekta ya Kahawa.

Anasema kuwa kwa upande wa Tanzania, utekelezaji huo umeanza kupitia Wizara ya Kilimo ambayo imezindua programu ya ujasiriamali kwa vijana uitwao Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT), moja ya mipango ikiwa ni kuanzisha
‘maduka ya kahawa yanayotembea’ ili kuchochea na kuongeza idadi ya watumiaji nchini.
Anaongeza kuwa migahawa hiyo, itawawezesha vijana wajasiriamali kujiajiri kwa kuuza kahawa katika maeneo mbalimbali ikiwemo barabarani kwa wapita njia, kwenye matukio ya umma na kijamii, vyuo vikuu na hospitali.
Pia, anasema serikali kupitia wizara ina mpango wa kuanzisha Vituo vya Umahiri vya Kahawa kwa kushirikiana na taasisi za elimu ya juu ili kuelimisha vijana kuhusu mnyororo mzima wa thamani wa kahawa kutoka uzalishaji hadi unywaji.
Anasema kuwa mpango wa kuanzisha mkutano wa nchi wazalishaji wa kahawa Afrika ni matokeo ya azimio
lililopitishwa wakati wa Mkutano wa 61 wa Mwaka wa IACO uliofanyika Kigali, Rwanda, Novemba 2021, la kuandaa mkutano wa ngazi ya juu wa nchi 25 zinazozalisha zao hilo Afrika ili kutathmini mapungufu na changamoto zinazosababisha kudumaa kwa wa Sekta ya Kahawa.
Baada ya kupitishwa kwa azimio hilo, mkutano wa kwanza ulifanyika Kenya Mei 2022, na ulipitisha ‘Tamko la Nairobi’, lililoazimia kuweka mkakati wa kuingiza kahawa kama bidhaa muhimu ya kimkakati katika Umoja wa
Afrika (AU) sambamba na Agenda 2063 ya AU.
Aidha, Bashe anasema Mkutano wa pili wa nchi wazalishaji wa kahawa Afrika uliofanyika Kampala, Uganda, Agosti 2023, ulipitisha ‘Tamko la Kampala’, lililokusudia kuwaomba Wakuu wa Nchi 25 zinazozalisha kahawa barani Afrika kuunga mkono kuidhinishwa na kujumuishwa kwa zao hilo kama bidhaa muhimu ya mkakati katika Ajenda ya 2063 ya AU na kuifanya IACO kuwa shirika maalumu la Umoja wa Afrika.
Katika kikao cha 37 cha kawaida cha Baraza Kuu la Umoja wa Afrika kilichofanyika Februari 2024, Addis Ababa, Ethiopia wakuu wa nchi na Serikali walipitisha kwa kauli moja kuingiza zao hilo kama bidhaa muhimu ya mkakati katika Agenda ya 2063 ya AU na kuifanya IACO kuwa shirika maalumu la Umoja wa Afrika.
Moja ya hatua zilizochukuliwa katika kutatua changamoto za biashara ya kahawa baina ya nchi za Afrika ni kuanzishwa kwa Mkataba wa Biashara Huria Afrika (AfCFTA) wa 2018 kwa lengo la kuondoa vikwazo vya biashara katika ya nchi za Africa na hivyo utekelezaji kamili wa mkataba huo utaimarisha biashara ya kahawa bila vizuizi baina ya nchi za Africa.
Mkutano huo wa tatu utajadili maeneo muhimu katika mnyororo wa thamani wa kahawa kwa ajili ya kufungua fursa za biashara na ajira kwa vijana.



