Serikali: Tutunze amani tusigeuke wakimbizi

SERIKALI imewataka vijana na wanaharakati watafute njia sahihi za kudai haki. Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene amesema hayo wakati wa mkutano wa pili unaohusisha serikali ya Tanzania, Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC) na Shirika la Kuhudumia Wakimbizi Duniani (UNHCR).
Wawakilishi wa pande hizo walitumia mkutano huo kusaini nyaraka zinazoelezea Mpango wa Urejeshwaji wa Wakimbizi 36,256 wa DRC. “Tunapozungumza mambo haya ya kuwaambia wenzetu warudi kwao na sisi huku hatuna nafasi ya kuwahifadhi, basi ni vizuri na sisi Watanzania tukajifunza somo hili kwamba tuna wajibu wa kutunza amani yetu ili na sisi kesho tusije kugeuka wakimbizi…,” alisema Simbachawene.
Ameongeza : “Kwa hiyo vijana na wale wote wanaharakati ambao wanafikiri njia ya vurugu na fujo na kuvunja amani ndio itakayowapa haki yao, hiyo njia ni ndefu mno. Tunazungumzia Congo iliyovurugika miaka thelathini iliyopita, amani yao haijarudi mpaka leo…” Simbachawene alisema kuna mfumo rasmi wa mazungumzo, kuweka hoja mezani lakini vurugu haijawahi kuisadia nchi yoyote.
“Ndugu zetu wa Congo tunao hapa wanaitafuta hiyo amani iliyopotea kwa miaka zaidi ya thelathini. Sisi Watanzania tuienzi amani yetu, tuilinde amani yetu, hususan vijana kwani ikipotea, hamtoiona ikirejea, muwe wavumilivu,” alisema. Wakimbizi 238,956 kutoka DRC wanahifadhiwa nchini, 152,019 wanatoka Burundi na mataifa mengine yakichangia wakimbizi 681. SOMA: Kimiti ahimiza haki, amani



