Serikali, wadau waombwa kuendelea kuboresha elimu

SERIKALI na wadau mbalimbali wa sekta ya elimu wameombwa kuendelea kuboresha sekta ya elimu nchini ili kujenga nchi yenye wasomi watakaosaidia kutatua changamoto mbalimbali ikiwemo mabadiliko ya tabia ya nchi.

Akizungumza mkoani Mtwara katika mahafali ya 13 ya Chuo kikuu kishiriki cha Stella Maris Mtwara yaliyofanyika kwenye Manispaa ya Mtwara Mikindani mkoani Mtwara, Mwalimu Mkuu wa chuo hicho Padri Thadeus Mkamwa amesema wadau hao waandae mitahala itayomjenga na kumuandaa mwanafunzi kwa kutatua matatizo ambayo hayategemewi kuwepo kama vile ukame, majanga ya moto pamoja na ajali za barabarani.

Aidha ya idadi ya wanafunzi wanaokuja kusoma mkoani Mtwara ni ndogo ukilinganisha na mikoa mingine hivyo ametoa wito kwa wadau wote wa elimu kushirikiana na serikali ya mkoa katika kuitangaza Mtwara kwenye sekta ya elimu kwa kuwapatia wanafunzi motisha ili kupata wanafunzi wengi mkoani humo na kupelekea kuongeza pato la mkoa na taasisi za elimu.

Advertisement

Pia amewataka wahitimu wote kuhakikisha kuwa elimu waliyoipata inakwenda kutatua changamoto za familia, jamii na taifa kwa ujumla.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dk Doto Biteko ambae ndie Mgeni rasmi katika Mahafali hayo amewataka wahitimu hao kila mmoja kusimamia na kuishi katika ndoto alizojiwekea ili kuhakikisha wanafikia malengo na kuacha kukata tamaa kwa kuangalia mafanikio ya wengine kwani kufanya hivyo kutapelekea kukata tamaa ya kusonga mbele.

“Wanajiuliza maswali mengi baada ya kuhitimu ni kitu gani kinafuata, wakati wote jihamasishe mwenyewe kila wakati jaribu kuwa watofauti, kaa kwenye mstari wako ndoto yako sio ndoto ya mwenzako”

“Ishikilie ndoto yako usigeuke kushoto wala kulia kuangalia ndoto ya mwenzio kwasababu kila mtu ana ndoto yake ya kuishi ukifanya hivyo utakosoea na matokeo yake utakuwa mtu wa kulalamika.”Amesema Biteko

Amesema kutokana na uhaba wa ajira kwa vijana serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imeamua kuimarisha sekta binafsi ili iwe nyenzo ya kutoa ajira kwa vijana hivyo amewataka wale watakaopata nafasi ya kuajiriwa kujiongezea maarifa, kufanya kazi kwa bidii na ubora ili kuendana na ushindani wa ajira.

Ameisisitiza kuwa, jamii ya Mtwara na wananchi wote kwa ujumla kujinyima na kuhakikisha wanawekeza kwenye elimu ili kupata maendeleo katika jamii zetu kwani hakuna miujiza ya maendeleo.

Odinya Peter ni Muhitimu katika mahafali hayo ambaye amewahasa wahitimu wenzake kutumia elimu waliyoipata kwa ajili ya kujiendeleza na kutosubiri ajira kutoka serikalini na badala yake waanze kujiajiri ili waweze kuwakomboa vijana wengine.