SIMIYU: KATIBU Mkuu wa chama cha ACT Wazalendo, Ado Shaibu amemshauri Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe kuwa mipango ya uwezeshaji wakulima inapaswa kujikita vijijini ili kuwawezesha wakulima kuongeza tija katika uzalishaji.
Akizungumza na wananchi wa Kata ya Banemhi Jimbo la Bariadi, Mkoani Simiyu Ado amesifu mradi wa BBT wa kuwezesha wakulima ila mradi huo ulipaswa kujikita zaidi vijijini.
“Kuna mradi huu wa BBT. Fikra ya kuwawezesha wakulima ni fikra njema, lakini, mpango ulipaswa kujikita vijijini waliko wakulima halisi”,amesema Ado.
Aliongezea kuwa “Mtindo wa wizara kukusanya vijana mijini, kuwapa mikopo, ardhi na nyenzo, hautaleta matokeo makubwa na mpango utafeli kama ilivyofeli mipango iliyotangulia ya kilimo,” alimalizia.
SOMA: https://www.kilimo.go.tz/
Katika hatua nyingine, Ado amesema kuwa ameishauri serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kubana matumizi na kuzuia ubadhirifu ili kuhakikisha kuwa inaajiri zaidi hasa kwenye maeneo ambayo yana mahitaji makubwa ya wafanyakazi kama vile walimu, madaktari na maofisa ugani.