MWANASHERIA Mkuu wa Serikali (AG) ,Hamza Johari amesema kukamilika kwa jengo la ofisi ya kanda pamoja na ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali mkoani Arusha kutawezesha utoaji huduma za kisheria kwa wananchi kwa karibu zaidi.
Ameyasema hayo wakati wa kutembelea ofisi ya Mwanasheria wa Serikali mkoani Arusha zilizopo ndani ya jengo la Mkuu wa Mkoa wa Arusha kisha kufanya ukaguzi wa jengo jipya la ghorofa linaloendelea kujengwa kwa gharama ya sh,bilioni 3.5 kata ya Sekei Jijini hapa.
Amesema ofisi hiyo itapambana kuhakikisha ujenzi wa jengo hilo unakamilika ili kuwezesha wanasheria kuwa na uwanda mpana wa utoaji huduma za kisheria kwa dhana ya kuwa na vituo jumuishi sanjari na ofisi za mkurugenzi wa mshtaka kwani Kanda ya Arusha inahudumia mikoa miwili yani Arusha na Manyara
“Jengo hili litakapokamilika tutaondokana na mazingira tuliyonayo kwa sasa ya kukaa kwenye jengo la ofisi ya mkuu wa mkoa hivyo tunatafuta fedha kwaajili ya kumalizia ujenzi awamu ya mwisho ili kusogeza huduma za sheria kwa wananchi”