Serikali yajivunia tija diplomasia ya uchumi
WIZARA ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imesema Tanzania inaadhimisha miaka 63 ya Uhuru wa Tanzania Bara ikiwa kwenye nafasi nzuri ya kidiplomasia.
Mkurugenzi wa Biashara ya Kimataifa na Diplomasia ya Uchumi katika wizara hiyo, Balozi John Ulanga amesema hali hiyo inachangiwa na uongozi bora, sera zenye mwamko wa maendeleo na ushirikiano wa kimataifa na kuongeza kuwa bado kuna fursa ya kufanya zaidi ya ilivyo sasa.
Balozi Ulanga aliieleza HabariLEO kuwa sera ya ‘Marafiki wa Wote’ imehakikisha kuwa Tanzania inashirikiana na mataifa mengi pasipo kuchagua kambi ya kisiasa na kwamba hiyo imeifanya kuaminika na mataifa mengine kutafuta suluhu za amani za nyumbani kwao.
“Tuna fursa kubwa ya kuimarisha mafanikio haya kwa kuhakikisha tunahamasisha uwekezaji endelevu na kujenga taswira ya taifa letu kama mshirika wa kimkakati wa maendeleo,” alisema.
Balozi Ulanga alisema Tanzania imekuwa ikitumia njia za kidiplomasia katika kusuluhisha migogoro barani Afrika ikiwa ni pamoja na kuwa mwenyeji wa mazungumzo ya amani kwa migogoro ya Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Aidha, alisema hivi sasa, diplomasia ya kiuchumi imekuwa kitovu cha sera za kigeni za Tanzania na imekuwa ikitumika uwekezaji wa kimataifa, kuimarisha biashara ya nje na kuvutia ushirikiano wa kiteknolojia ili kuchochea maendeleo ya ndani.
Balozi Ulanga alisema uwekezaji katika sekta za kilimo, utalii, miundombinu na nishati vimekuwa kielelezo cha mafanikio yaliyopatikana kutokana na msisitizo uliowekwa na serikali katika kuimarisha diplomasia ya uchumi.
Alitaja mafanikio mengine kuwa ni kuongezeka kwa idadi ya watalii wanaoingia nchini kwa zaidi ya asilimia 20, hasa kutokana uhamasishaji ulifanywa na Rais Samia Suluhu Hassan kupitia filamu ya ‘Tanzania: The Royal Tour’.
Aidha, alisema ziara za Rais Samia Suluhu Hassan na viongozi wengine wakuu zimezaa matunda kwa kufungua masoko ya kimataifa kwa bidhaa za Tanzania, hasa za kilimo na kuvutia wawekezaji wanaokuja kutoka nje.
Alisema kuimarika kwa diplomasia ya uchumi na kuboresha kwa mazingira ya biashara kumechangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la thamani ya miradi inayoandikishwa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kila mwaka.
Balozi Ulanga alisema kwa mujibu wa TIC thamani ya miradi inayoandikishwa imekuwa ikongezeka mwaka hadi mwaka ambapo kwa mwaka huu, miradi yenye thamani ya Dola za Marekani zaidi ya bilioni 6.5 imeshaandikishwa.
Alisema mafanikio katika diplomasia ya uchumi yametokana na sababu kadhaa ikiwemo uongozi kipaumbele cha serikali, ushirikiano wa kimataifa na matumizi ya rasilimali asili.
Alifafanua kuwa serikali imeamua kuifanya diplomasia ya uchumi kuwa ajenda ya kitaifa kupita sera na sheria zinazoimarisha mazingira ya biashara.
Alisema pia mikataba na wawekezaji wa kimataifa imechochea uwekezaji katika sekta za msingi kama kilimo, nishati na teknolojia na kuongeza kuwa nchi imefanikiwa kutumia rasilimali zake kama madini na vivutio vya utalii kuvutia wawekezaji wa kigeni.



